Zero! Hakuna mbunge aliyepatikana na coronavirus— Muturi

Muturi
Muturi
Hakuna mbunge  au mfanyikazi wa bunge aliyepatikana na virusi vya Corona katika vipimo vya hiari vilivyofanywa mapema mwezi huu.

Spika wa bunge Justin Muturi  katika arifa kwa wabunge amesema  matokeo ya waliopimwa kutoka bunge  na seneti pamoja na wafanyikazi  wa mabunge yote yameonyesha kwamba hakuna aliyepatikana na virusi hivyo.

“  Ningependa kusisitiza kwamba matokeo haya hayafai kutufanya tulegeze kamba kuhusu jitihada za kudumisha usafi  na kuwa na tahadhari  pamoja na kuvalia barakoa  na kuepuka maeneo yaliyo na misongamano.’  Muturi alishauri.

Vipimo vya hiari vya wabunge na wafanyikazi wa bunge vilifanywa kati ya Aprili tarehe 2 na tarehe 4 katika majengo ya bunge.

Bunge liliwataka wajumbe na wafanyikazi kufanyiwa vipimo kwa hiari  kama jitihada za mapema za kukabiliana na ugonjwa huo  baada ya ripoti za magazeti kudai kwamba wabunge 17 wamepatikana na virusi hivyo.

Muturi amesema  tume ya wafanyikazi wa bunge inandaa  vipimo vinginge kwa wabunge na wafanyikazi wa bunge na wanafaa kuendelea kufuata ushauri na mwongozo unaotolewa na shirika la afya duniani WHO na wizara ya Afya nchini

“ Shughuli hiyo itakuwa ya hiari na inawalenga wabunge wote  na wafanyikazi. Wengine watakaopimwa ni wafanyikazi waliopewa kandarasi ya kufanya kazi ya usafi bungeni. ‘ Muturi aliongeza