Moto ndani ya Jubilee! Wanawake wa 'tanga tanga' walalamikia vitisho

ALICE WAHOME
ALICE WAHOME

Kundi moja la wanawake wanachama wa chama tawala cha Jubilee wamelalamikia vile katibu mkuu wa chama hicho alitumia ubaguzi kuandikia barua wanawake maseneta wateule waliosusia mkutano ulioitishwa na rais Uhuru Kenyatta na kuandaliwa katika ikulu ya Nairobi.

Wanawake hao wabunge wametaja hatua hiyo kama vitisho kufuatia hatua ya baadhi ya maseneta kukosa kuhudhuria mkutano uliongozwa na rais Kenyatta.

Ni katika mkutano huo wa Ikulu ambapo iliafikiwa kuwaondoa maseneta Kipchumba Murkomen na Susan Kihika kotoka nyadhifa zao za kiongozi wa wengi na kiranja wa wengi katika seneti mtawalia.

Nyadhifa zao zilichukuliwa na seneta wa West Pokot Samuel Poghisio na seneta wa Murang'a Irungu Kang'ata mtawalia.

"Pia tunakataa na kukashifu hatua haramu ya katibu mkuu wa chama na katika seneti pamoja na kupuuzwa kwa sheria ya vyama vya kisiasa ili pafanyike shughuli halali ," wanawake hao walisema katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Pia walielezea kutoridhishwa na hatua ya kuondolewa kwa kiranja wa kike na nafasi hiyo kupewa mwanamume.

"Hii inaashiria nini kuhusu wanawake wanavyochukuliwa katika chama chetu?" Wabunge hao walihoji.

"Tunataka chama chetu kuacha mara moja vitisho dhidi ya wanachama wa kike ambao wamefanya mengi nyakati ngumu kukuza chama."

Viongozi hao walisema kwamba wanawaunga mkono Kihika na Murkomen na maseneta wote wateule ambao walipewa barua za kuadhibiwa.