Gavana wa Kirinyaga aliye mashakani baada ya wawakilishi wa kaunti yake kupiga kura ya kumuondoa afisini sasa anatafuta msaada wa kiongozi wa ODM Raila Odinga ili kujinasua kutoka kwa masaibu yake.
Licha ya bwana Odinga kukanusha kwamba alikutana na Waiguru siku ya Alhamisi wiki jana, kuna juhudi kwa upande wa washirika wa gavana huyo kuhakikisha kwamba chama cha ODM Kinamsaidia asiondolewe mamlakani wakati hoja hiyo itakapowasilishwa katika seneti.
Odinga mwishoni mwa wiki alitoa taarifa kukanusha kwamba alifanya mkutano na gavana Waiguru hatua ambayo sasa huenda ikaashiria kwamba atapambana kivyake kujinasua kwani hatma yake sasa ipo katika mikono ya maseneta.