Kuna nini? Kemri, KNH zakoma kuwapima wananchi virusi vya corona

Endapo ulitaka kupimwa corona bure basi uatapata tatizo kwa sababu serikali imezuia maabara kubwa  zilizokuwa zikitumiwa kufanya vipimo hivyo.

Wizara ya afya imechukua hatua hiyo ili kupambana na ufisadi na sasa  kituo cha  huduma za Maabara  kwa umma, Kenyatta National Hospital (KNH)  na shirika la utafiti wa matibabu KEMRI haziruhusiwi tena kupima corona.

Memo iliyotolewa kwa wakuu wa vitengo mbalimbali  imeonyesha pia kwamba hospitali ya Mbagathi iliyokuwa ikitumiwa pia kufanya vipimo sasa haitawachukua watu wanaoshukiwa kuwa virusi hivyo bali itawalaza tu wale ambao tayari wamethibitishwa kuwa na virusi vya corona.

Kemri,  kwa upande wake imetangaza kwamba haitakuwa ikikusanya sampuli za  covid 19  na badala yake  itakuwa ikizipima sampuli kutoka vituo maalum vilivyopewa idhini ya  kuchukua sampuli.

Wakenya sasa watategemea makundi maalum ya dharura yatakayokusanya sampuli  kutoka kwa mashirika na vituo maalum  ambayo yatataka huduma za kupimwa na kuwekwa katika karantini.