COVID 19 : WHO yasema mataifa yanachukua mkondo hatari katika vita dhidi ya virusi vya Corona

Janga la corona  litazidi kuwa baya zaidi na hatari  ikiwa serikali zitashindwa kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na ugonjwa huo,  limetoa tahadhari Shirika la afya duniani (WHO).

Mkuu wa shirika hilo Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema ''nchi nyingi sana (zilikua) zikielekea kwenye njia isiyo sahihi.''

''Idadi ya watu walioambukizwa ilikuwa ikiongezeka kwenye maeneo ambayo masharti yalikuwa hayafuatwi'', aliongeza.

Amerika kwa sasa imekuwa kitovu cha janga.

Marekani imeshuhudia ongezeko la maambukizi wakati kukiwa na mvutano kati ya wataalamu wa afya na Rais Donald Trump.

Marekani, nchi iliyoathirika zaidi duniani, ina watu zaidi ya milioni 3.3 walioathirika na vifo zaidi ya 135,000 kwa mujibu wa Chuo cha Johns Hopkins.

Katika mkutano wa siku ya Jumatatu , Dkt Tedros amesema ''ujumbe mchanganyiko kutoka kwa viongozi'' umekuwa ukishusha uaminifu wa Umma katika jitihada za kudhibiti janga la virusi vya corona.

''Virusi vinaendelea kuwa adui wa kwanza wa watu, lakini hatua za serikali nyingi na watu hazioneshi hilo,'' alisema.

Dkt Tedros amesema kuwa hatua kama vile ya kukaa mbali na mwingine, kunawa mikono na kuvaa barakoa katika mazingira yanayolazimu kufanya hivyo zilipaswa kuzingatiwa kwa kiasi kikubwa, akitahadharisha kuwa kutakuwa na ''hakuna kurejea kwenye maisha ya zamani siku za usoni''.

''Ikiwa vitu vya msingi havifuatwi, kuna njia moja janga hili litaelekea,'' dkt aliongeza: ''hali itakuwa mbaya na mbaya sana.''

Dkt Mike Ryan mkurugenzi wa dharura ndani ya WHO, amesema kuwa kulegeza masharti ya kutotoka nje katika nchi za Amerika na kufungua baadhi ya maeneo kumesababisha maambukizi kwa kiasi kikubwa''.

Amerika ya Kusini imethibitisha kuwa zaidi ya watu 145,000 wamepoteza maisha kutokana na virusi vya corona, ingawa idadi inaaminika kuwa zaidi kwa sababu ya upimaji usio thabiti.

Nusu ya idadi ya vifo hivyo ni kutoka Brazil, ambako Rais Jair Bolsonaro amekwenda kinyume na masharti ya kupambana na kusambaa kwa virusi.

Dkt Ryan amesema kufunga miji mikubwa kungekuwa na athari kubwa za kiuchumi, lakini marufuku ya kutotoka nje katika baadhi ya maeneo inaweza kuwa muhimu ili kudhibiti kusambaa kwa virusi.

Ametaka serikali kuweka mipango ''madhubuti'', akiongeza : ''Raia wanapaswa kuelewa, na inapaswa kuwa rahisi kufuata masharti yanayowekwa.''

''Tunapaswa kujifunza kuishi na virusi,'' alisema Dkt Ryan, akitahadharisha kuwa matarajio kuwa virusi vinaweza kuondoshwa, au chanjo kuwa tayari, ndani ya miezi kadhaa ''hakuna uhalisia''.

Amesema kuwa haijajulikana bado kama kupona ugonjwa wa Covid-19 kutasababisha kuwa na kinga, au kama ni hivyo, ni kwa muda gani kinga hiyo itakuwepo mwilini.

Utafiti uliotolewa siku ya Jumatatu na wanasayansi katika Chuo cha kings jijini London umesema kuwa kinga dhidi ya virusi inaweza isiwe ya muda mrefu.Wanasayansi katika chuo hicho walifanyia utafiti watu 98 ili kuelewa namna gani mwili hupambana na virusi , na kwa muda gani kinga hii huwepo ndani ya majuma kadhaa na miezi baada ya kupona ugonjwa wa Covid-19.