Kenya ina maseneta 67 huku 47 wakiwa waliochaguliwa na 20 wakiteuliwa bungeni na vyama mbalimbali. Magavana wana mamlaka zaidi na pia wanasiamia kiasi kikubwa cha raslimali kuliko maseneta ambao mshahara wao kila mwezi ni takriban shilingi laki sita pamoja na marupurupu mengine.
Magavana takriban 20 wanahudumia mihula yao ya kwanza huku wengine 21 wakiwa katika mkondo wa lala salama baada ya kuhudumu kipindi cha kwanza.
Miongoni mwa wanaokamilisha hatamu zao ni mwenyekiti wa baraza la magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Hassan Joho (Mombasa), Okoth Obado (Migori), Josphat Nanok (Turkana) na Jackson Mandago (Uasin Gishu).
Maseneta Johnson Sakaja (Nairobi), Fred Outa (Kisumu), Ochillo Ayacko (Migori), Irungu Kang'ata (Murang’a), James Orengo (Siaya) na Cleophas Malala (Kakamega) wote wametangaza nia zao kutaka kuwa magavana .
Wengine ni Steward Madzayo (Kilifi), Ledama Olekina (Narok), Kithure Kindiki (Tharaka Nithi), Aaron Cheruiyot (Kericho), Samson Cherargei (Nandi), Enoch Wambua (Kitui) na Susan Kihika (Nakuru).
Wengi zaidi hawataki kutangaza nia zao mapema lakini tayari wameanza mikakati ya kujitayarisha kuwania viti hivyo.
Wadadisi wanasema kinachowavutia wengi kutaka kuwa magavana ni mamlaka, ushawishi na raslimali ambazo magavana wanasimamia.
“Pesa na maamlaka ni vitu viwili vinavyowapa msukumo zaidi . kila mtu anapigania kuingia kuliko na pesa ,hata katika uchaguzi mkuu uliopita wachache sana walitaka kuwa maseneta kwa sababu haina fedha ,maseneta hawasimamii raslimali zozote’ anasema mchanganuzi Martin Andati