Naibu wa rais amekuwa akijitangaza kama sauti na mtetezi wa watu maskini na ameamua kuzungumza moja kwa moja na wananchi huku akimuacha Uhuru kusalia kama kiongozi mwenye mamlaka yanayoonekana ya kurithi kutoka kwa familia. Wanaomshauri Ruto wanaamini kwamba anaweza kupata kura za kutosha katika maeneo ya kati, Lower Eastern, Magharibi, Pwani na Kaskazini mashariki ili kuchukua hatamu za uongozi mwaka wa 2022.
DP ambaye ametimuliwa kutoka ngome za mamlaka amekuwa akitoa misaada kwa biashara ndogo ndogo ili kujitangaza kwamba anayajali maslahi yao na kupandisha hadhi yake machoni pa watu wengi wa kawaida. Wanaojua undani wa mango huo wanasema washirika wa Ruto wamechakura utafiti wa shirika la takwimu nchini kuhusu mambo ya uchumi na wanatumia takwimu hizo ili kujua kero za wananchi na kuahidi kuzishughulikia kupitia njia mbalimbali ikiwemo kuwapa misaada inayotolewa na kambi ya Ruto.
Kwa mfano ripoti hiyo iligundua kwamba maeneo ya Mlima Kenya,Nairobi, Nyanza na Rift Valley yana idadi ya juu ya wafanyibiashara wadogo wadogo. Walifaulu katika shughuli zao bila kutegemea utajiri wowote wa kifamilia na wanakumbana na changamoto nyingi sana ikiwemo kunaswa kwa mali za wafanyibiashara wengi wanaoagiza bidhaa kutoka nje katika msako dhidi ya bidhaa za ubora wa chini ama ghushi, kundi la Ruto linategemea kutumia malalamishi kama hayo ili kujenga uungwaji mkono miongoni mwa watu. Washirika wa Ruto wanasema baadhi ya biashara zinatoa upinzani kwa zile zinazomilikiwa na watu kutoka familia zenye ushawishi mkubwa kisiasa na ndio kwa sababu zililengwa na mashirika ya serikali. Mbunge wa Belgut Nelson Koech ambaye ni miongoni mwa wanaofanya kazi kwa karibu sana na DP ameliambia gazeti la The Star kwamba vuguvugu la ‘hustler Nation’ litakuwa kubwa kuliko migawanyiko ya kikabila bali litategemea dhana na fikra za kibiashara miongoni mwa wakenya .
Washirika wa Raila hata hivyo wamepuuza mbinu hiyo ya Ruto wakisema haitamsaidia Ruto kupata kura katika uchaguzi mkuu ujao. Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi ameutaja mkakati huo kama wa ‘kushangaza kwa sababu hauna nafasi katika siasa za Kenya’.