Uhuru ataka wakenya kuiga mfano wa KDF

Muhtasari

• Fuateni kielelezo cha ustadi wa Jeshi la Ulinzi nchini katika utoaji huduma.

• Rais alipongeza Jeshi la ulinzi nchini kwa utaalamu wake ambao umelisaidia kuhudumia taifa kwa njia ya kipekee.

• Rais alipuuzilia mbali madai kwamba kuhusisha Jeshi la Ulinzi katika utoaji huduma ni kulifanya taifa kuwa la kijeshi.

 

Rais Uhuru Kenyatta amewataka Wakenya wanaofanya kazi katika sekta mbalimbali za uchumi  kuiga mfano wa utendakazi bora wa Jeshi la Ulinzi nchini, akisema hatua hiyo itahakikisha utoaji bora wa huduma na kwa wakati unaofaa.

Wakati huo huo, Rais alipongeza Jeshi la ulinzi nchini kwa utaalamu wake ambao umelisaidia kuhudumia taifa kwa njia ya kipekee.

“Iwapo sote nchini Kenya tutatenda na kuonyesha tabia; na kulipenda na kuitumikia nchi yetu kwa njia ambayo Jeshi la Ulinzi linavyofanya, leo hii Kenya ingelikuwa taifa kuu. Na sote tuna mengi ya kujifunza,” Alisema Rais Kenyatta.

Uhuru alisema hayo siku ya Jumanne katika gereji ya Shirika la Huduma kwa Jiji  kuu la Nairobi iliyo katika eneo la viwandani alipozindua magari 83  ambayo yalirekebishwa na shirika hilo la serikali.Shirika hili lilirekebisha magari hayo kwa gharama ya shilingi 22 milioni kwa kipindi cha miezi miwili kufuatia kutolewa kwa gereji hiyo kwa shirika hilo kutoka kwa Serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Magari hayo  yalikuwa yameachwa katika gereji hiyo kama vyuma kuu kuu kwa miaka mingi. Magari hayo ni pamoja na malori 21 ya aina ya Tipa, magari 24 ya kuzima moto, magari sita ya kubebea wagonjwa, majukwaa matatu ya kuwashia taa za barabarani, magari mawili ya kusugua na kusafisha barabara na tingatinga mbili za kutengeneza barabara miongoni mwa vifaa vingine vilivyokuwa vimeachwa hapo kwa miaka minane.

Rais Kenyatta alielezea matumaini yake kwamba magari 80 yaliyosalia yakiwa yameharibika katika gereji hiyo yatarekebishwa katika miezi miwili ijayo tayari kuhudumia wakaazi wa Nairobi.

Wakati huohuo, Rais alipuuzilia mbali madai kwamba kuhusisha Jeshi la Ulinzi katika utoaji huduma ni kulifanya taifa kuwa la kijeshi.

“Sina nia kama hiyo, (kulifanya taifa kuwa la kijeshi). Lakini ni mjinga pekee ambaye hawezi kuwatumia wale wanaoweza kuchapa kazi kumsaidia kutimiza malengo yake...Silifanyi taifa kuwa la kijeshi. Nawatumia wakenya wa kutegemewa kutimiza ajenda yangu  kwa Jamhuri hii. Na jeshi la KDF ni sehemu ya raia wetu,” kasema Rais.

Rais alitoa mfano wa miradi kadha ya muundomsingi ikiwemo kukarabatiwa kwa reli, bandari ya Kisumu na kufufuliwa kwa meli kama  baadhi ya mafanikio ya hivi karibuni ya jeshi la KDF.