Vijana waliouawa 2 walinyongwa, 1 alipigwa na kifaa butu-Upasuaji

Muhtasari
  • Mhasiriwa wa nne hakuchunguzwa, kwani mwili wake ulikuwa umesalia mifupa tu
  • Daktari mkuu wa upasuaji wa serikali Johansen Oduor aliendesha upasuaji katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City Mortuary  mnamo Alhamisi
  • Alisema mchakato wa kumtambua mwathiriwa wa nne wa kiume utachukua muda
Image: DCI

Ripoti ya upasuaji wa mili ya vijana ilinaonyesha kuwa vijana ambao walitekwa nyara na baadaye kuuawa na muuaji aliyekiri walinyongwa na kupigwa kichwani na kitu butu.

Upasuaji ulionyesha  Brian Omondi na Junior Mutuku walinyongwa, wakati Charles Were Opindo alipata majeraha ya kichwa yaliyotokana na kifaa butu.

Mhasiriwa wa nne hakuchunguzwa, kwani mwili wake ulikuwa umesalia mifupa tu.

Daktari mkuu wa upasuaji wa serikali Johansen Oduor aliendesha upasuaji katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City Mortuary  mnamo Alhamisi.

Alisema mchakato wa kumtambua mwathiriwa wa nne wa kiume utachukua muda.

Wazazi wa Omondi hawakuweza kutambua mwili wake kwa kuwa ulikuwa umeoza vibaya, na kusababisha maafisa kuchukua sampuli zao kwa uchunguzi wa DNA.

Uchunguzi utatafuta pia ikiwa wavulana walilawitiwa kabla ya kuuawa.

Miili mitatu ilikusanywa kutoka eneo la Kabete kaunti ya Kiambu, wakati wa nne, mifupa, ilipatikana katika kisima katika eneo la Pumwani jijini Nairobi.

Mhemko ulishuhudiwa  katika chumba cha kuhifadhia maiti wakati mtu mmoja alionekana, akisema binti yake, mwenye umri wa miaka minane, alipotea tangu Februari na anashuku kuwa ni mwathiriwa wa muuaji, Masten Milimo Wanjala, mwenye umri wa miaka 25.

Wanjala na binamu yake wamekamatwa kwa mauaji hayo. Haya yanajiri wakati polisi wakiendelea kutafuta miili zaidi ya vijana waliopotea baada ya kutekwa nyara na kuuawa na Wanjala.

Polisi waliruhusiwa mnamo Julai 15 na korti kumshikilia Wanjala kwa siku 30.

Wanjala anadai aliteka nyara na kuua watoto wasiopungua 12 katika miaka minne huko Nairobi, Machakos na Bungoma. Miili minne tu imepatikana.