"Kwani kuna serikali ngapi Kenya?" Gavana Ngilu akosoa Ruto kwa kuomba bwenyenye wa Uturuki msamaha

Ngilu amemkosoa naibu rais kwa kile anasema ni kuendeleza serikali nyingine kando na serikali tawala inayoongozwa na rais Uhuru Kenyatta.

Muhtasari

•Gavana Ngilu alikuwa anatoa hisia zake kufuatia ujumbe ambao Ruto alichapisha mtandaoni akidai kuwa alikuwa amepigia Harun Aydin na kumuomba msamaha kwa sababu ya kuteswa kwake na kubandikwa jina 'gaidi'.

•Ruto alikosoa kukamatwa na kufurusha nchini kwa bwenyenye Aydin Harun ambaye ni mshirika wake wa karibu na kudai kuwa kitendo hicho ni cha kisiasa na chaweza kusababisha madhara kwa uchumi wa nchi.

Naibu rais William Ruto na gavana Charity Ngilu
Naibu rais William Ruto na gavana Charity Ngilu
Image: HISANI

Gavana wa Kitui Charity Ngilu amekosoa hatua ya naibu rais William Ruto kuomba bwenyenye wa Uturuki msamaha kwa niaba ya serikali.

Ngilu amemkosoa naibu rais kwa kile anasema ni kuendeleza serikali nyingine kando na serikali tawala inayoongozwa na rais Uhuru Kenyatta.

Gavana Ngilu alikuwa anatoa hisia zake kufuatia ujumbe ambao Ruto alichapisha mtandaoni akidai kuwa alikuwa amepigia Harun Aydin na kumuomba msamaha kwa sababu ya kuteswa kwake na kubandikwa jina 'gaidi'.

"Ala! Kwani kuna serikali ngapi huku Kenya? Bwana DP, unaomba msamaha kwa niaba ya serikali ipi haswa?" Ngilu alimuuliza Ruto kupitia mtandao wa Twitter.

Kulingana na Ngilu, serikali rasmi ya Kenya ndiyo iliyomkamata bwana Aydin  kwa madai kuwa yeye ni mfadhili wa magaidi.

Ngilu alisema kuwa matendo ya naibu rais yanasababisha hali ya mkanganyiko serikalini, kote nchini na nje ya taifa.

"Serikali ya Kenya ndiyo ilimkamata mshukiwa wa kufadhili magaidi. Hali ya mkanganyiko ambayo umekuwa ukipanda serikalini na kote nchini sasa umeanza kuiuza kwa washirika wetu wa biashara?" Ngilu aliendelea kusema.

Ruto alikosoa kukamatwa na kufurusha nchini kwa bwenyenye Aydin Harun ambaye ni mshirika wake wa karibu na kudai kuwa kitendo hicho ni cha kisiasa na chaweza kusababisha madhara kwa uchumi wa nchi.

"Nilizungumza tu na kuomba msamaha kwa niaba ya GoK kwa Aydin Harun, ambaye sasa yuko Uturuki, ambaye alikamatwa kisiasa, aliteswa na kutajwa uwongo kama" gaidi "lakini baadaye akaulizwa kutoka nchini tusiwashtumu wale wanaohusika. Uchumi mdogo wa kisiasa ni ghali / hatari na utaharibu uchumi wetu," Ruto aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.