Mwanamke na wanawe 4 waliouawa kikatili na mumewe wafanyiwa mazishi ya kihisia Kirinyaga

Muhtasari

•Watano hao wanadaiwa kukumbana na kifo chao cha ghafla mikononi mwa kiongozi wa familia hiyo Paul Murage Njuki ambaye anadaiwa kuwaua kikatili kwa kutumia silaha hatari mwishoni mwa mwezi uliopita nyumbani kwao Gichugu.

Masanduku yenye mabaki ya mama na watoto wake wanne waliokatwakatwa hadi kufa mwishoni mwa mwezi uliopita yakionyeshwa wakati wa hafla ya mazishi yao katika kijiji cha Karwagi huko Mwea
Masanduku yenye mabaki ya mama na watoto wake wanne waliokatwakatwa hadi kufa mwishoni mwa mwezi uliopita yakionyeshwa wakati wa hafla ya mazishi yao katika kijiji cha Karwagi huko Mwea
Image: WANGECHI WANG'ONDU

Wingu la simanzi lilitanda  katika kijiji cha Karwagi, eneo la Mwea Mashariki Kaunti ya Kirinyaga wakati wa hafla ya mazishi ya mama mmoja na watoto wake wanne waliouawa kwa kukatwakatwa na mapanga mwishoni mwa mwezi uliopita.

Waombolezaji wengi walishindwa kudhibiti machozi walipoona majeneza matano ya Millicent Muthoni 38 na watoto wake wadogo watano wenye umri wa kati ya mwaka 1 hadi 13.

Mchungaji aliyekuwa anaongoza ibada Cyrus Ngera alijaribu kufariji waombolezaji waliohudhuria mazishi hayo yaliyoonekana kujaa hisia huku akiwasihi wajipe moyo.

"Tuombee familia huku tukiendelea kutafuta haki kwa ndugu zao waliofariki,” alisema.

Kakake Muthoni, Patrick Njiru alimtaja marehemu kuwa mwenye upendo na mwenye kujali. Alimlimbikizia sifa marehemu dadake akimtaja kama mkulima aliyekuwa na  bidii kubwa.

Kwa hayo alisema walikuwa karibu sana kutokana na uhusiano wao wa damu na mahusiano sawa ya biashara ya kilimo.

"Mbali na kuwa wanafamilia, tulijadiliana kuhusu jinsi tungeweza kupanua kilimo chetu na akaja na mawazo bora ambayo yalikuwa muhimu katika biashara zetu."

"Mbali na hilo, yeye pamoja na watoto walinitembelea mara kwa mara nyumba yangu ambayo haiko mbali sana na walipokuwa wanaishi, ambapo tungetumia muda mwingi tukiwa na uhusiano wa kifamilia na kwa hilo, nitawapeza sana," alisema.

Mbunge wa Gichugu, Gichimu Githinji alisema ataandaa kongamano la kuelimisha umma ambapo ataleta wataalam wa saikolojia na ushauri nasaha ili kutoa msaada wa kihisia unaohitajika kwa wapiga kura wake.

"Katika juhudi za kuzuia matukio kama haya mabaya yasitokee siku zijazo, nitahakikisha kwamba ninaleta wanasaikolojia na wataalamu wa magonjwa ya akili ili kutoa ujuzi wa kihisia na msaada kwa familia nyingi zinazopitia mambo magumu ya ndoa au kihisia." Gichimu alisema. Pia aliahidi kuendelea kusaidia familia kwa njia zozote za kifedha kadri anayoweza.

Marehemu walizikwa katika kaburi la pamoja ambalo lilichimbwa na mchimbaji iliyetolewa na serikali ya kaunti.

Watano hao wanadaiwa kukumbana na kifo chao cha ghafla mikononi mwa kiongozi wa familia hiyo Paul Murage Njuki ambaye anadaiwa kuwaua kikatili kwa kutumia silaha hatari mwishoni mwa mwezi uliopita nyumbani kwao Gichugu.

Pia inadaiwa kuwa mshtakiwa alimnajisi binti yao mkubwa kabla ya kumuua.

Njuki ambaye Jumatano alifikishwa mbele ya mahakama kuu ya Kerugoya hakusomewa mashtaka kwa kukosa uwakilishi wa kisheria.

Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Januari 24, 2022 kwa kuwa iliidhinisha serikali kumpatia wakili kabla ya tarehe hiyo.

(Utafsiri: Samuel Maina)