Naibu chifu auwa na mkewe kwa kisu Kirinyaga

Polisi wanaendelea kumhoji mke wa marehemu ili kusaidia katika uchunguzi.

Muhtasari

•Wanandoa hao walikuwa na watoto wawili wadogo na wamekuwa wakiishi kwa amani bila kuwepo kwa mizozo ya kifamilia hapo awali.

Crime scene
Crime scene

Habari na Wangechi Wangond'u

Wingu la simanzi limetanda katika eneo ndogo la Kiamugumo, kaunti ya Kirinyaga baada ya naibu chifu kupatikana akiwa ameuawa kwa kisu.

Denis Njeru 36, ambaye hajahudumu kwa kipindi kirefu  anaripotiwa kudungwa na mkewe hadi kifo mwendo wa saa nne usiku wa Jumatano kufuatia mzozo wa kinyumbani usiojulikana.

Rose Njeru, ambaye ni mama ya marehemu na mjumbe wa kuteuliwa katika kaunti ya Kirinyaga alisema wamekuwa wakiishi pamoja na familia ya mwanawe.

"Tulimsikia mke wa mwanangu akipiga kelele mwendo wa saa nne usiku akisema kwamba alikuwa amemchoma kisu mumewe wakiwa jikoni kwa bahati mbaya. Tulikimbia pale tukamkuta Njeru akiwa amelala chini huku akipiga kelele na kutokwa na  damu kwenye jeraha la kisu" Alisema Bi Njeru.

Alieleza jinsi walimchukua mwanawe na kumkimbiza katika hospitali ya rufaa ya Kerugoya ambapo alitangazwa kufariki alipofika.

Bi Njeru alisema wanandoa hao walikuwa na watoto wawili wadogo na wamekuwa wakiishi kwa amani bila kuwepo kwa mizozo ya kifamilia hapo awali.

Polisi wanaendelea kumhoji mke wa marehemu ili kusaidia katika uchunguzi.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya jamaa mwingine, Paul Murage kuua familia yake yote (mkewe na watoto wanne)  katika kijiji cha Kathata, kaunti hiyo hiyo ya Kirinyaga.