Jamaa aua mkewe na watoto wanne katika tukio la kutisha Kirinyaga

Muhtasari

•Baada ya kutekeleza  unyama huo alijisalimisha kwa polisi kisha kuelekeza wapelelezi hadi eneo alikokuwa ametupa silaha za mauaji na nyumbani ambako mili ya wahasiriwa ilikuwa.

•Miili ya marehemu ilipatikana juu ya vitanda vyao na polisi wanasema bado hawajabaini kilichopelekea mauaji hayo.

Crime scene photo
Crime scene photo

Siku ya Jumatatu polisi katika kaunti ya Kirinyaga walimkamata mwanaume mmoja kufuatia tuhuma za kuua mkewe na watoto wanne katika hali tatanishi.

Jamaa huyo anayefahamika kama Paul Murage Njuki (35) anadaiwa kunajisi binti yake mmoja kabla ya kumuua.

Baada ya kutekeleza  unyama huo alijisalimisha kwa polisi kisha kuelekeza wapelelezi hadi eneo alikokuwa ametupa silaha za mauaji na nyumbani ambako mili ya wahasiriwa ilikuwa.

Watoto hao ni wa umri kati ya mwaka mmoja na 13.

Polisi wanasema mshukiwa alitumia silaha butu na panga kutekeleza mauaji hayo.

Walisema mshukiwa aliua watoto wawili wa kiume na binti wawili kabla ya kutupa silaha ya mauaji kwa kichaka kilicho karibu na mto ulio katika kijiji cha Kathata.

 

Wahasiriwa walitambulishwa kama Millicent Muthoni Rungu 38, Nelly Wawira 13, Gifton Bundi Muthoni 13, Sheromit Wambui Muthoni 5, na Clifton Njuki Murage wa mwaka mmoja.

Silaha moja ya mauaji na mkata zilipatikana katika eneo la tukio.

Mshukiwa aliambia polisi alitupa shoka ambayo alitumia kwenye kichaka na msako ukaanzishwa.

Gari la polisi ambalo lilikuwa linasafirisha mili lilikwama matopeni kwa masaa kadhaa kufuatia hali mbaya ya barabara na mvua kubwa katika eneo hilo.

"TUKIO LA KUTISHA"

Waathiriwa walikuwa na majeraha vichwani na mmoja wa watoto wa kiume alikuwa na majeraha ya moto mguuni kuashiria kuwa alimchoma.

Shahidi alieleza tukio hilo kuwa la kutisha. Kikosi cha wapelelezi kilitumwa Jumanne kwenye eneo hilo ili kuwasaidia wale waliokuwa wanafanya uchunguzi.

Wenyeji waliambia polisi mwanamume huyo alionekana mpweke na kusumbuliwa katika siku za hivi majuzi.

Haijabainika kama alikuwa na ugomvi na familia hiyo na ni nini kilianzisha ugomvi huo.