"Ni ndoto iliyotimia!" Muturi asherehekea uteuzi wake kama mwanasheria mkuu

Alisema ni kitu ambacho amekuwa akitamani kila wakati.

Muhtasari

•Muturi aliteuliwa kuhudumu katika wadhifa huo na Rais William Ruto mnamo Jumanne wakati alipokuwa akitaja Baraza lake la Mawaziri.

•Alijiunga na timu ya Kwanza Alliance mnamo Aprili 9, 2022

Spika Justin Muturi wakati wa kikao na wanahabari katika Klabu ya United Kenya Nairobi Jumanne 11, Januari.
Spika Justin Muturi wakati wa kikao na wanahabari katika Klabu ya United Kenya Nairobi Jumanne 11, Januari.
Image: WILFRED NYANGARESI

Iwapo itahakikiwa na kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa, Justin Muturi atakuwa Mwanasheria Mkuu wa nane wa Kenya.

Muturi aliteuliwa kuhudumu katika wadhifa huo na Rais William Ruto mnamo Jumanne wakati alipokuwa akitaja Baraza lake la Mawaziri.

Siku ya Alhamisi, spika huyo wa zamani hakuweza kuficha furaha yake kufuatia uteuzi huo. Alisema ni kitu ambacho amekuwa akitamani kila wakati.

Akizungumza katika majengo ya bunge baada ya hotuba ya Ruto ya kuapishwa katika Bunge hilo, alisema ana furaha kuhudumu katika nafasi tofauti.

"Nimefurahi, kwangu ni ndoto iliyotimia. Nimeanza kutoka Mahakama, kwenda Bungeni kama Mbunge na kisha Spika. Naona ni fursa kwangu kutoa utumishi katika mfumo tofauti wa serikali," alisema. alisema.

Alijiunga na timu ya Kwanza Alliance mnamo Aprili 9, 2022, katika kile kinachoonekana kuwa tikiti ya dhahabu kujiunga na baraza la mawaziri linalofuata.

Kabla ya uteuzi huo, Muturi alihudumu kama Spika wa Bunge la Kitaifa tangu 2013 wakati huo Rais Uhuru Kenyatta na Ruto walichukua wadhifa huo.

Mnamo 2017, Uhuru alipochaguliwa tena, Muturi aliendelea kuhudumu kama Spika hadi Septemba 15, 2022, ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Moses Wetang'ula.