Ruto 'achagiza' miaka 60 ya Uhuru Uganda, atoa wito wa ushirikiano zaidi

Rais alihimiza ushirikiano zaidi wa nchi za Afrika Mashariki, akimtaka Rais Museveni kuongoza hilo.

Muhtasari

•Ruto ni miongoni mwa viongozi kutoka mataifa mbalimbali walioungana na mamilioni ya raia wa Uganda wanaodhimisha miaka 60 ya Uhuru wa taifa hilo jana.

•Rais Museveni katika hotuba yake ya kurasa 30, na yeye alihimiza umuhimu wa kuunganisha nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, ili kujenga uchumi imara.

Image: TWITTER// WILLIAM RUTO

Rais wa Kenya, William Ruto ni miongoni mwa viongozi kutoka mataifa mbalimbali walioungana na mamilioni ya raia wa Uganda wanaodhimisha miaka 60 ya Uhuru wa taifa hilo jana.

Wiki iliyopita rais wa Uganda, Yoweri Museveni aliwaomba radhi wakenya kutokana na machapisho ya mtoto wake mkubwa, Jenerali Muhoozi Kainerugaba aliyeandika kupitia mtandao wa twitter kwamba jeshi lake lingeweza ‘kuiteka Nairobi baada ya wiki mbili tu’.

Machapisho hayo yaliibua hasira miongoni mwa wakenya.

Akizungumza leo katika sherehe za maadhimisho hayo zilizofanyika katika uwanja wa Kololo na kupambwa na gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama vya Uganda, Ruto alihimiza ushirikiano zaidi wa nchi za Afrika Mashariki, akimtaka Rais Museveni kuongoza hilo.

'Tunaweza kutengeneza ustawi na kuunganisha fursa katika nchi zetu kwa faida ya watu milioni 300 Afrika mashariki na watu bilioni 1.2 katika bara la Afrika', alisema Ruto.

Kabla ya kumkaribisha Ruto, Rais Museveni katika hotuba yake ya kurasa 30, na yeye alihimiza umuhimu wa kuunganisha nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, ili kujenga uchumi imara.

Alisisitiza pia kuendelea na ujenzi wa bomba la mafuta linalounganisha Uganda na Tanzania, licha ya Umoja wa Ulaya kukosoa ujenzi wake kwa sababu za mazingira.

Mbali na Ruto, viongozi wengine waliohudhuria sherehe hizo za miaka 60 ya uhuru wa Uganda ni pamoja na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit, Rais wa Somalia Hamad Sheikh Muhamud, Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi aliyemuwakilisha Rais Samia Suluhu wa Tanzania na wawakilishi wengine kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo DRC, Mali na Rwanda.

Tangu ipate uhuru wake mwaka 1962 kutoka kwa wakoloni, Uganda imetawaliwa na viongozi kadhaa, lakini Museveni peke yake akitawala kwa miaka 36, akikosolewa zaidi kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyotajwa kukithiri nchini humo. Mara nyingi amekuwa akikanusha tuhuma hizo.