Waziri Nakhumicha amtembelea mwanahabari Catherine Kasavuli hospitalini na kumuombea

Kasavuli amelazwa katika hospitali hiyo tangu Oktoba 26

Muhtasari

•Waziri Nakhumicha pia alichukua fursa hiyo kuwatembelea wagonjwa wengine katika hospitali hiyo na kusikiliza malalamishi yao.

amtembelea mwanahabari mkongwe Catherine Kasavuli katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta jijini Nairobi. Tarehe 22 Desemba 2022.
Waziri wa Afya Susan Nakhumicha amtembelea mwanahabari mkongwe Catherine Kasavuli katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta jijini Nairobi. Tarehe 22 Desemba 2022.
Image: TWITTER// CS NAKHUMICHA

Siku ya Alhamisi Waziri wa Afya Susan Nakhumicha alimtembelea mtangazaji mkongwe wa televisheni Catherine Kasavuli katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta.(KNH)

Kasavuli anaendelea kupokea matibabu baada ya kugunduliwa kuwa na ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi mapema mwaka huu.

"Nilimtembelea mtangazaji mkongwe Catherine Kasavuli ambaye anaendelea kupata nafuu katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta na kumuombea aendelee kupata nafuu," Waziri alisema.

Waziri huyo ni miongoni mwa wageni wengi ambao Kasavuli amekuwa nao kwa muda wa miezi miwili iliyopita tangu alazwe huku akiendelea kufanyiwa matibabu.

Waziri Nakhumicha pia alichukua fursa hiyo kuwatembelea wagonjwa wengine katika hospitali hiyo na kusikiliza malalamishi yao.

"Nilisikiliza maoni yao kuhusu huduma za matibabu katika KNH, tutafanyia kazi maoni haya," alisema.

Katika ujumbe wake kwenye ukurasa wake wa Instagram, Kasavuli alisema yeye ni mwanamke shupavu huku akiwashukuru watu wanaomuombea.

"Najua nitapambana na hili. Kwa sasa ninajiandaa kwa utaratibu wa awamu ya pili," alisema.

Kasavuli amelazwa katika hospitali hiyo tangu Oktoba 26.

Ziara ya Nakhumicha inakuja takriban wiki  tatu baada ya waziri wa Masuala ya Vijana, Michezo na Sanaa Ababu Namwamba kumtembelea mwanahabari huyo mkongwe.

Namwamba alimtembelea Kasavuli mapema mwezi huu ili kumfariji mtangazaji huyo wa habari gwiji na kusali naye.

"Umetia moyo kizazi cha watangazaji wakuu wa kike. Ushawishi wako kwa wanahabari wetu wa kike hauwezi kulinganishwa kamwe. Mungu akupe uponyaji ili uendelee kuwashauri wasichana wetu,” Namwamba alisema wakati wa ziara ya hospitali.

Waziri pia alimuomba Kasavuli kuwa na kikao naye baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.