Msanii wa Mugithi aliyempoteza mwanawe kwenye ajali ya basi la Easy Coach azungumza

Mwanafunzi wa Chavakali Boys ambaye aliangamia kwenye ajali ya basi iliyotokea Jumatatu usiku ametambuliwa.

Muhtasari

•Mwimbaji Kareh B alieleza jinsi alivyopata habari kuhusu ajali hiyo kupitia mitandao ya kijamii usiku wa kuamkia Jumanne

•Alibaini kuwa mwanawe aliaga baada ya wanafunzi wengine kufika Nairobi Jumanne asubuhi, lakini mwanawe akakosa kufika.

alimpoteza mwanawe katika ajali iliyotokea Mamboleo, Kisumu.
Kareh B alimpoteza mwanawe katika ajali iliyotokea Mamboleo, Kisumu.
Image: HISANI

Mwanafunzi wa shule ya upili ya Chavakali Boys ambaye aliangamia kwenye ajali ya barabarani iliyotokea siku ya Jumatatu usiku ameweza kutambuliwa.

Ajali hiyo iliyohusisha basi la kampuni ya Easy Coach lililokuwa likiwasafirisha wanafunzi kuelekea nyumbani kwa likizo ya Aprili ilitokea katika eneo la Mamboleo, kaunti ya Kisumu mwendo wa saa tatu usiku wa kuamkia Jumanne. Wanafunzi kadhaa walijeruhiwa huku mwanafunzi mmoja aliyetambulika kwa jina la Joseph Maduli akiaga dunia.

Imebainika kuwa mvulana huyo mwenye umri wa miaka 17 ni mtoto wa staa wa nyimbo za Mugithi Mary Wangari Gioche ambaye anajulikana zaidi kama Kareh B.

Mwimbaji Kareh B alizungumza na Citizen TV siku ya Jumanne ambapo alieleza jinsi alivyopata habari kuhusu ajali hiyo kupitia mitandao ya kijamii usiku wa kuamkia Jumanne. Alisema kuwa yeye pamoja na wazazi wengine  tayari walikuwa wameeleza wasiwasi wao kuhusu wanafunzi hao kusafiri usiku, lakini ndio ulikuwa mpango pekee wa safari ambao shule iliweza kuwaandalia wanafunzi hao.

“Sikupata usingizi. Mwendo wa kati ya saa sita unusu na saa saba usiku, habari kwenye mitandao ya kijamii. Hapo ndo nilipata ujumbe kwamba basi ambayo imeanguka ya Chavakali,” alisema Kareh B.

Mwimbaji huyo alisema alikuja kujua kwamba mwanawe alifariki katika ajali hiyo siku ya Jumanne asubuhi, saa kadhaa baada ya ajali hiyo kutokea.

Alibaini kuwa mwanawe aliaga baada ya wanafunzi wengi waliosafiri kutoka Kisumu hadi Nairobi kufika Nairobi Jumanne asubuhi, lakini mwanawe akakosa kufika.

“Nilianza kujiuliza mbona wangu hajafika. Nikiuliza mmoja wa waalimu ambaye alisema alikuwa kwenye eneo la ajali, ananiambia wale ambao walipata majeraha kidogo walipewa ruhusa ya kupigia wazazi wao wawaambie usiwe na wasiwasi niko hospitalini niko sawa,” alisema.

Wanafunzi wengine wawili waliojeruhiwa vibaya kwenye ajali hiyo wanaendelea kupokea matibabu maalum katika hospitali moja mjini Kisumu wakati wengine 32 waliopata majeraha madogo wakiwa walipata matibabu katika hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga.