Wanawake wawili wauawa kinyama na mshukiwa wa wizi Meru

Shahidi Muthomi Mburugu alisema marehemu walimuona mshukiwa akivamia karakana hiyo na kabla hawajapiga mayowe kuitisha msaada.

Muhtasari

• Miili hiyo ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Kanyakine.

Polisi na wakaazi katika eneo ambapo miili ya wanawake wawili waliouawa katika eneo la Kiigene huko Nkubu, kaunti ya Meru mnamo Aprili 16, 2024. Picha: GERALD MUTETHIA
Polisi na wakaazi katika eneo ambapo miili ya wanawake wawili waliouawa katika eneo la Kiigene huko Nkubu, kaunti ya Meru mnamo Aprili 16, 2024. Picha: GERALD MUTETHIA

Wanawake wawili wenye umri wa kati ya miaka 25-30 waliuawa Jumanne asubuhi na mshukiwa wa wizi wa mbao eneo la Kiigene huko Nkubu, Imenti Kusini, Meru.

Shahidi Muthomi Mburugu alisema kuwa marehemu walimuona mshukiwa akivamia karakana hiyo na kabla hawajapiga mayowe kuitisha msaada, mshukiwa aligundua kuwa walikuwa wamemwona ndipo akawavamia.

“Tumesikitishwa na mauaji ya kikatili ya wanawake wawili, tumeshtushwa sana kuwapoteza vijana wa aina hii, nilisikia mayowe barabarani lakini sikuweza kusaidia kwa wakati, niliona miili yao ikiwa imelala barabarani,” Mburugu alisema.

Mburugu alivitaka vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina utakaofanikisha kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa huyo.

Msaidizi wa chifu wa Kiigine Joseph Muthuri alikashifu mauaji hayo na kuhakikishia umma kuwa utawala wake utahakikisha muuaji huyo ameadhibiwa.

"Wawili hao walikuwa na umri wa kati ya miaka 25-30. Mshukiwa aliyewaua alionekana na wanawake wawili waliofariki akivunja karakana ili kuiba. Tutahakikisha tunamkamata mshukiwa," Muthuri alisema.

"Natoa wito kwa majirani ambao wanaweza kuwa na taarifa muhimu zinazoweza kusababisha kukamatwa kwa watu hao washirikiane nasi kumpata mtuhumiwa," alisema.

Miili hiyo ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Kanyakine.