Mazungumzo ya Trump kubadilisha uchaguzi yanaswa

Muhtasari

• Mazungumzo ya Trump ya siri Georgia kujaribu kubadilisha uchaguzi yanaswa.

• Joe Biden alishinda uchaguzi wa Georgia pamoja na majimbo mengine muhimu.

• "Nataka tu kupata kura 11,780," Bwana Trump alimwambia katibu wa chama cha Republican Brad Raffensperger jimboni humo.

Rais wa Marekani Donald Trump amerekodiwa akimwambia afisa mkuu wa uchaguzi Georgia atafute kura za kutosha kuwezesha kubadilishwa kwa matokeo ya uchaguzi.

"Nataka tu kupata kura 11,780," Bwana Trump alimwambia katibu wa chama cha Republican Brad Raffensperger jimboni humo katika mazungumzo yaliyorekodiwa na kutolewa na gazeti la Washington Post.

Bwana Raffensperger anasikika akijibu kuwa matokeo ya uchaguzi ya Georgia yalikuwa sawa.

 

Joe Biden alishinda uchaguzi wa Georgia pamoja na majimbo mengine muhimu na kumwezesha kupata kura 306 za wajumbe dhidi ya Bwana Trump aliyepata kura 232.

Tangu uchaguzi uliofanywa Novemba 3, Bwana Trump amekuwa akidai kuwa kura ziliibwa bila kutoa ushahidi wowote unaothibitisha madai yake.

Majimbo yote 50 yamethibitisha matokeo ya uchaguzi huo baadhi ya vituo ikiwa ni baada ya kura kuhesabiwa tena au pia kwasababu ya kesi zilizowasilishwa mahakamani kupinga matokeo.

Hadi kufikia sasa, Marekani imetupilia mbali kesi 60 zilizokuwa zimewasilishwa kupinga ushindi wa Bwana Biden.

Aidha bunge linatarajiwa kuidhinisha rasmi matokeo ya uchaguzi huo Januari 6.

Bwana Biden wa chama cha Democrat, anatarajiwa kuapishwa kama rais wa Marekani Januari 20.

Pia, wapiga kura huko Georgia wanatarajiwa kupiga tena kura Jumanne kuchagua maseneta wawili wa jimbo hilo na matokeo ya uchaguzi huo huenda yakaweka sawa jinsi nguvu ya uongozi itakavyokuwa katika bunge la Seneti.

Ikiwa washindani wawili wa chama cha Democrat watashinda, kunamaanisha kwamba kutakuwa na idadi sawa ya wabunge wa vyama vya Republican na Democratic na makamu mteule wa chama cha Democratic Kamala Harris ndiye atakayekuwa na usemi katika kura ya kufanya maamuzi.

Bwana Biden wa chama cha Democrat tayari anadhibiti bunge la wawakilishi.

Nini kilichotokea katika simu ya Trump?

Katika kipande kilichotolewa na gazeti la Washington Post, Bwana Trump anasikika akisema pengine njia nyingine ni kumshawishi na kumshinikiza katibu wa jimbo la Georgia.

Alisisitiza kuwa ameshinda uchaguzi katika jimbo la Georgia na kumuambia Bwana Raffensperger kwamba hakukuwa na ubaya wowote kusema kuwa "mumehesabu kura tena".

Bwana Raffensperger alijibu kwa kusema: "Changamoto uliyonayo Mheshimiwa Rais ni kwamba takwimu ulizonazo wewe ni za uwongo."

Baadaye katika simu hiyo, Bwana Trump alisema uvumi uliopo ni kuwa kura zilizopigwa kwa njia ya posta zimeharibiwa na mashine ya kupiga kura iliondolewa kutoka kaunti ya Fulton jimboni humo - dai ambalo wakili wa Bwana Raffensperger amesema sio sahihi.

Aidha, baadaye rais alimtishia afisa huyo na kumtajia njia anazoweza kuchukua kisheria.

"Unajua walichofanya na husemi lolote. Huo ni uhalifu. Huwezi kuacha hilo litendeke ukiwa kimya. Hiyo ni hatari kubwa kwako wewe na kwa Ryan, wakili wako," Bwana Trump alisema.

Kisha akaitisha kura za ziada 11,780 - ambazo zitafanya awe na jumla ya kura 2,473,634 jimboni humo, moja zaidi ya kura alizopata Bwana Biden, 2,473,633.

Aliamuambia Bwana Raffensperger achunguze tena matokeo ya uchaguzi ya jimbo hilo.

"Unaweza kuyachunguza tena lakini yafuatilie na watu ambao wanataka kupata majibu, wala sio wasiotaka kupata ufumbuzi," alisema.

"Bwana Rais, unao watu wako wanaowasilisha taarifa na tuna watu wetu wanaowasilisha taarifa vilevile na kisha baada ya hapo yanafikishwa mahakamaani ambayo itafanya uamuzi," Raffensperger aljibu. "Lazima tutetee nambari zetu na tunaamini kuwa takwimu zetu ziko sahihi.

Hata hivyo Bwana Raffensperger hakutoa maelezo yoyote kuhusu ulaghai unaodaiwa na rais. "Hana taarifa yoyote!" Rais aliandika.

Bwana Raffensperger akajibu: "Kwaheshima, Rais Trump: Unachosema sio kweli. Ukweli utajitokeza."

 

Ikulu ya Marekani haijasema lolote kuhusu mazungumzo yaliyovuja.

Afisa wa juu wa Democrat Adam Schiff amesema: Kwa mara nyingine tena. "Jaribio la Trump kuingilia demokrasia liko wazi. Kupitia sauti iliyorekodiwa."

Mwanasiasa wa Republican mwenye msimamo wa kati Adam Kinzinger ameandika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akisema: "Bila shaka hii inachukiza. Kila mbunge anayefikiria kupinga matokeo ya uchaguzi huu, hawezi kufanya hivyo kwa nia moja."

Je matokeo ya uchaguzi yataidhinishwa lini?

Kuna mgawanyiko katika chama cha Republican baada ya maseneta 12 kusema kuwa hawatapiga kura kuidhinisha ushindi wa Bwana Biden katika kikao cha bunge la seneti Januari 6.

Ted Cruz aliongoza maseneta 11 akiitisha kucheleweshwa kwa mchakato huo kwa siku 10 ili kuchunguza madai ya wizi wa kura.

Makamu Mike Pence - ambaye kama rais wa bunge la Seneti anatarajiwa kusimamia kikao hicho na kumtangaza Bwana Biden mshindi amesema anaunga mkono hatua hiyo.

Bwana Pence hakurejelea madai ya wizi wa kura lakini mkuu wa wafanyakazi alisema Bwana Pence atashirikisha wengine kile anachosema ni "wasiwasi wa mamilioni ya Wamarekani kuhusu wizi wa kura na udanganyifu".

Seneta wa Missouri Josh Hawley pia amesema kuwa atapinga matokeo ya uchaguzi kwasababu ya madai ya ukosefu wa uadilifu.

Wakati huohuo, maseneta wanne akiwemo Mitt Romney wametia saini taarifa inayosema watapiga kura kuidhinisha ushindi wa Bwana Biden.

BBC