Wakenya wote nchini Ukraine wako salama, Wizara ya Mambo ya Nje yasema

Muhtasari
  • Kupitia misheni yake mjini Vienna, serikali ilitoa dokezo la tahadhari kwa Wakenya wote nchini Ukraine
Waziri wa mambo ya nje Omamo
Image: Maktaba

Serikali ya Kenya, kupitia Wizara ya Mashauri ya Kigeni, imesema kuwa raia wa Kenya walio nchini Ukraini wako salama.

Kupitia misheni yake mjini Vienna, serikali ilitoa dokezo la tahadhari kwa Wakenya wote nchini Ukraine.

“Kufikia sasa Wakenya wote nchini Ukraine wameripotiwa kuwa salama. Baadhi ya Wakenya hata hivyo wamekwama katika maeneo ya mpaka, haswa na Poland ambapo kwa sababu ya vizuizi vya viza wameshindwa kuvuka,” Wizara ilisema.

Wakenya pia wameshauriwa kufanya tathmini kuhusu hali zao na kuchukua tahadhari zinazofaa na au kufanya mipango ya kuondoka wanavyoona inafaa kulingana na hali zao.

Wizara ilisema kwamba inawasiliana na mataifa yote jirani ya Ukraini ndani ya Umoja wa Ulaya kutafuta makao na kuwaruhusu Wakenya kupita katika nchi zao iwapo wanataka kurejea nyumbani.

Iliongeza kuwa sehemu ya magharibi ya Ukrainia iko salama kwa sababu kuna shughuli ndogo sana za kijeshi zinazoendelea huko.

Pia, Wakenya wamehimizwa kubaki huko huku wakisubiri hali itulie na au wanapopanga mipango yao ya kurejea nyumbani.