Bobi Wine kuandaa tamasha la kuchangisha pesa kuwaokoa Waganda waliokwama Uarabuni

Kama tunavyojua, mamia ya Waganda wamekwama katika nchi hizi bila msaada - Bobi Wine

Muhtasari

• “Mapato kutoka kwa tamasha hilo yataenda kusaidia Waganda ambao wamekwama katika vituo vya kizuizini huko Dubai na Nchi zingine za Kiarabu" - Wine.

Kionozi wa Uganda Bobi Wine kuandaa tamasha la kuchangisha pesa kuwaokoa waganda waliokwama Uarabuni
Kionozi wa Uganda Bobi Wine kuandaa tamasha la kuchangisha pesa kuwaokoa waganda waliokwama Uarabuni
Image: Facebook

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine ametangaza kuandaa tamasha kubwa linalonuiwa kuchangisha pesa ili kuwasaidia raia wan chi hiyo haswa kina dada waliokwama katika mataifa ya Uarabuni huko Mashariki ya Kati.

Wine ambaye kwa muda mrefu alikuwa mwanamuziki kabla ya kutia guu kwenye siasa alisema kupitia kurasa zake za mitandaoni kwamba tamasha hilo kubwa litafanyika mubashara na mapato yote yataenda moja kwa moja kuwasaidia kuwasaidia Waganda ambao wamekwama uarabuni kwa kukosa namna ya kurudi nyumbani.

“Tunatangaza Tamasha Linalolenga Kuchangisha Pesa za Kusaidia Watu Wetu Waliokwama Dubai na Nchi nyingine za Kiarabu. Kama tunavyojua, mamia ya Waganda wamekwama katika nchi hizi bila msaada. Wengi wao wanataka kurudi nyumbani lakini hawana pesa za kuwezesha safari zao kurudi nyumbani,” Wine aliandika.

Alisema tamasha hilo litafanyika tarehe 8 Octoba katika moja ya kumbi mashuhuri huko Dubai. Alisema kwa sababu idadi ya watu wanaolilia msaada wa kutaka kurudi nyumbani ni wengi, huenda mapato hayo hayatatosha kuwakimu wote ila katika siku za usoni, watatangaza mbinu zingine za kuwawezesha wahisani wema kutoa michango yao pia ili kuwakwamua Waganda walioko ‘Utumwani’ katika mataifa ya Kiarabu.

“Mapato kutoka kwa tamasha hilo yataenda kusaidia Waganda ambao wamekwama katika vituo vya kizuizini huko Dubai na Nchi zingine za Kiarabu zikiwemo Saudi Arabia, Qatar na Oman. Wacha tujitokeze kwa wingi na tufanye sababu kuwa ya maana,” Wine aliwarai watu.

Hatua hii ya Wine imekuja siku chache baada ya Wakenya kuzua mitandaoni wakilalama kuhusu wapendwa wao kuteswa katika mataifa hayo ya Kiarabu huku ubalozi wan chi ukiwa umefyata.