Waziri wa leba auawa kwa kupigwa risasi na mlinzi wake

Taarifa zilisema kuwa mlinzi huyo baadae pia alijigeuzia mtutu wa bunduki na kujifyatulia risasi.

Muhtasari

• “Ndiyo. Nenda kwa Kyanja, kuna risasi. Mwanajeshi amempiga risasi bosi wake,” Naibu msemaji wa polisi wa Metropolitan ya Kampala Luke Owoyesigire alithibitisha

Mwanafunzi ajiua kwa kujipiga risasi Kilimanjaro
Mwanafunzi ajiua kwa kujipiga risasi Kilimanjaro
Image: YoutubeScreengrab

Waziri wa leba wa nchini Uganda Charles Okello Engola amepigwa risasi na kuuawa na mlinzi wake.

Kulingana na jarida la Daily Monitor, Naibu msemaji wa polisi wa Metropolitan ya Kampala Luke Owoyesigire alithibitisha kisa hicho.

Waziri huyo aliuawa katika boma lake eneo la Kyanja viungani mwa jiji la Kampala.

“Ndiyo. Nenda kwa Kyanja, kuna risasi. Mwanajeshi amempiga risasi bosi wake,” Owoyesigire aliambia gazeti la Daily Monitor katika mahojiano mafupi ya simu.

Spika wa Bunge la Uganda, Bi Anita Among, pia alithibitisha kifo cha waziri huyo alipokuwa akiongoza kikao cha mashauriano leo asubuhi.

“Leo asubuhi, nilipata taarifa za kusikitisha kuwa Mhe Engola amepigwa risasi na mlinzi wake na baadae akajipiga risasi. Roho yake ipumzike kwa amani. Huo ulikuwa mpango wa Mungu. Hatuwezi kubadilisha chochote,” Bi Among alisema.

Eneo la uhalifu limezingirwa na maafisa wa usalama.

 Hata hivyo, haijulikani sababu ya mlinzi huyo kuchukua uamuzi huo ambao umewaacha wengi katika hali ya mshangao.

Kwa kawaida, taarifa za mlinzi kumshambulia bosi wake ni nadra sana kutokea.

 

Waziri wa Jinsia, Betty Amongi ni miongoni mwa maafisa wa serikali ambao tayari wamefika nyumbani kwa Engola huko Kyanja.