Museveni amteua mtoto wake kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi

Jenerali Muhoozi alikuwa akihudumu nafasi ya mshauri mkuu wa Rais katika masuala ya operesheni maalumu.

Muhtasari

• Aliyekuwa mkuu wa majeshi Jenerali Wilson Mbasu Mbadi ameteuliwa kuwa Waziri wa biashara katika mabadiliko mapya ya safu ya Baraza la mawaziri nchini Uganda.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amemteua mtoto wake, Jenerali Muhoozi Kainerugaba kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF).Gazeti la Daily Monitor la Uganda limeripoti.

Anachukua nafasi ya Jenerali Wilson Mbasu Mbadi ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa biashara katika mabadiliko mapya ya safu ya Baraza la mawaziri lililotangazwa karibuni.

Jenerali Muhoozi alikuwa akihudumu nafasi ya mshauri mkuu wa Rais katika masuala ya operesheni maalumu.

Kwingineko,

Makamu wa Rais wa Tanzania Philip Mpango ametishia kujiuzulu kutokana na tatizo la maji la muda mrefu linalowaathiri wakazi wa wilaya ya Mwanga kaskazini.

Bw Mpango aliwashutumu wakandarasi wanaofanya kazi katika mradi mkubwa unaolenga kusambaza maji katika eneo hilo kwa kuchukua muda mrefu kuukamilisha.

''Mradi huu umekuwa ni kero kwa wananchi wa maeneo haya tunayoyasema. sasa imefika wakati wanachi hawa wapate maji'' alisema.

Mradi huo wa thamani ya zaidi ya $100,000 (£79,000) ulianzishwa karibu miaka 20 iliyopita, kulingana na Bw Mpango.

"Kama mradi huu hautakuwa unatoa maji [kwa wenyeji] ifikapo Juni, nitaacha kazi. Sijui nini itakuwa hatima ya msimamizi wa eneo hilo na wasaidizi wake ikiwa nitaacha kazi," Bw Mpango alisema.

“Siwezi kuja hapa tena na kuwaambia wananchi wasubiri zaidi maji haya, maji ni uhai,” aliongeza.

Kulingana na maafisa wa serikali walioandamana na Bw Mpango hadi Mwanga siku ya Alhamisi, mradi huo umekamilika kwa karibu 90%.