Mshtuko baada ya bilionea aliyetangazwa kufa miaka 3 iliyopita kupatikana akiishi na mpenziwe Urusi

Mara ya mwisho alionekana akitembea peke yake asubuhi moja na hakurudi tena hotelini kwake.

Muhtasari

•Haub alikuwa akifanya mazoezi ya mbio za kupanda milima kwenye mlima wa Matterhorn nchini Uswizi alipotoweka Aprili 2018.

•Haub  anadaiwa kupiga simu ya Veronika mara 13 ndani ya siku tatu kabla ya kutoweka kwake mnamo 2018.

Bilionea Karl-Erivan Haub
Image: HISANI

Uchunguzi umefichua maelezo ya kushtua kwamba bilionea wa Kijerumani mwenye asili ya Marekani, Karl-Erivan Haub ambaye inaaminika alikufa mwaka wa 2018 baada ya kutoweka wakati akijivinjri nchini Uswizi anaishi na mwanadada wa Urusi katika mji wa Moscow.

Haub, ambaye alikuwa na umri wa miaka 58 wakati alipodaiwa kufariki, alikuwa akifanya mazoezi ya mbio za kupanda milima kwenye mlima wa Matterhorn nchini Uswizi alipotoweka Aprili 2018.

Mara ya mwisho alionekana akitembea peke yake asubuhi moja na hakurudi tena hotelini kwake.

Mamlaka ikiwa ni pamoja na timu za waokoaji  na helikopta tano walitafuta kwa siku sita, lakini hakupatikana, wala mwili wake.

Baada ya miaka mitatu, mnamo 2021, alitangazwa rasmi kuwa amekufa na mahakama ya Ujerumani. Alidaiwa kuacha mke wake, watoto wawili, na kampuni yake, kampuni kubwa ya rejareja ya Tengelmann Group iliyokuwa na wafanyikazi zaidi ya 75,000.

Kaka yake mdogo,  Christian aliapa mahakamani kwamba hakuna dalili yoyote Karl-Erivan, ambaye thamani yake ilikadiriwa kuwa pauni bilioni 5.2 alikuwa hai.

Lakini sasa uchunguzi mkubwa unaoongozwa na mtangazaji wa Ujerumani RTL unadai kuwa Karl-Erivan alipatikana jijini Moscow - na inaaminika kuwa anaishi huko na mwanadada aitwaye Veronika Ermilova.

Haub, ambaye sasa angekuwa na umri wa miaka 64, anadaiwa kupiga simu ya Veronika mara 13 ndani ya siku tatu kabla ya kutoweka kwake mnamo 2018.

Simu hizo zilikuwa za muda mrefu - moja iliyochukua zaidi ya saa moja - na kusababisha tuhuma kwamba alikuwa akipanga njama ya kudanganya kifo chake.

Uchunguzi uligundua kuwa Veronika, 44, aliendesha wakala wa matukio yasiyoonekana wazi.

Mwandishi wa habari wa RTL, Liv von Boetticher alikisia kwamba kutoweka kwa Karl-Erivan nchini Uswizi kunaweza kuwa kumetokana na biashara zisizo halali.

Njia kamili iliyotumiwa na Karl-Erivan kutekeleza madai yake ya kutoweka haijulikani.

Baadhi wanaamini kwamba bilionea huyo wa Ujerumani aliteremka kwenye milima ya Alps na kuenda hadi Italia, lakini hakuna maelezo ya mahali alipo baada ya kuanza safari yake ya kuteleza akiwa peke yake.