Mahakama ya muachilia MCA wa Korogocho bila masharti

Hakimu mkuu wa Milimani Gilbert Shikwe aliagiza polisi kumwachilia Odhiambo mara moja.

Muhtasari

• Polisi walimtaka MCA huyo azuiliwe ili wakamilishe uchunguzi kuhusu madai kwamba alitoa maneno ambayo huenda yakazua ghasia au kuyumbisha taifa. 

MCA wa Korogocho Absalom Odhiambo katika Mahakama ya Milimani baada ya kuachiliwa bila masharti mnamo Februari 1, Picha: DOUGLAS OKIDDY
MCA wa Korogocho Absalom Odhiambo katika Mahakama ya Milimani baada ya kuachiliwa bila masharti mnamo Februari 1, Picha: DOUGLAS OKIDDY

Mahakama ya Nairobi imetupilia mbali ombi la polisi lililotaka kumweka kizuizini mwakilishi wadi wa Korogocho Absalom Odhiambo kwa siku saba kusubiri uchunguzi wa kesi inayodaiwa kuwa ya matamshi ya chuki.

Hakimu mkuu wa Milimani Gilbert Shikwe alisema maombi yaliyowasilishwa hayakuzingatia masharti yoyote ya kisheria.

Aliagiza polisi kumwachilia Odhiambo mara moja.

"Nimeangalia kesi iliyowasilishwa mahakamani. Niliangalia uamuzi wa Mahakama Kuu, kifungu cha 96A cha kanuni ya adhabu ni kinyume cha katiba na nimebaini kuwa uamuzi huo haujapingwa na upande wa mashtaka," Shikwe alisema.

"Ni ukweli usiopingika kwamba mwombaji anayeomba amri ya kumweka kizuizini mshukiwa kwa siku saba hana msingi kisheria kufanya hivyo."

"Anaachiliwa bila masharti pengine kama amezuiliwa kinyume cha sheria."

Aidha Hakimu huyo alimsuta Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kulala kazini na kushindwa kuwasilisha marekebisho ya sheria kama ilivyoelekezwa na majaji wa Mahakama Kuu.

Asubuhi, mawakili wa utetezi wakiongozwa na Danstan Omari walisimamisha uamuzi huo baada ya kuwasilisha maombi mengine.

Kesi ya uchochezi dhidi ya MCA ilichukua mwelekeo mpya baada ya wakili Danstan Omari kuwasilisha mahakamani kwamba Kifungu cha 96A cha Kanuni ya Adhabu ambayo MCA alikamatwa chini yake, ni kwa mujibu wa sheria ya maamuzi ya majaji watatu iliyotolewa mwaka 2015.

Kulingana na upande wa utetezi, mwanasiasa Johnstone Muthama mwaka wa 2015 alipinga uhalali wa kikatiba wa mashtaka ya uchochezi kama inavyoelezwa katika kifungu hicho cha Kanuni ya Adhabu ambapo majaji wa Mahakama ya Juu waliagiza Bunge lifutilie mbali kifungu hicho.

mbele ya hakimu Gilbert Shikwe alifikishwa katika Mahakama ya Milimani kwa matamshi ya uchochezi aliyoyatoa wakati wa mkutano wa Azimio Jumapili Januari 31.
MCA wa Korogocho Absalom Odhiambo mbele ya hakimu Gilbert Shikwe alifikishwa katika Mahakama ya Milimani kwa matamshi ya uchochezi aliyoyatoa wakati wa mkutano wa Azimio Jumapili Januari 31.
Image: DOUGLAS OKIDDY

Hata hivyo, kifungu hicho bado hakijarekebishwa hivyo kosa la matamshi ya chuki halitambuliki tena kisheria, mahakama iliambiwa. 

"Sehemu ambayo mteja wangu alikamatwa na kuletwa hapa inaonyesha kuwa mahakama haina shughuli yoyote kwa mujibu wa uamuzi wa Mahakama Kuu kushikilia MCA hata kwa sekunde moja" wakili huyo alisema. 

Katika ombi lililowasilishwa kortini, polisi walimtaka MCA huyo azuiliwe ili wakamilishe uchunguzi kuhusu madai kwamba alitoa maneno ambayo huenda yakazua ghasia au kuyumbisha taifa. 

Polisi walidai kuwa walihitaji siku saba kupata uchochezi wowote unaowezekana, ujumbe kutoka kwa simu yake na kurekodi taarifa kwa serikali ili kuongeza ushahidi kwa upande wa mashtaka. Odhiambo alikamatwa alipokuwa akisubiri kuzungumza na maafisa wa Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa katika afisi zao za Upper Hill. 

Alikuwa anasubiri kurekodi taarifa. Tume hiyo ilikuwa imemwita Odhiambo kuhusu matamshi aliyotoa wakati wa mkutano wa viongozi wa mashinani wa Azimio ulioandaliwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga Jumatano wiki jana. Akizungumza wakati wa maandamano hayo, Odhiambo anadaiwa kutumia maneno ya uchochezi.Alimwomba Raila awaruhusu kwenda Ikulu na kumtoa Ruto kwa nguvu.

"Nataka tuingie town, tufunge biashara. Hakuna biashara itaendelea hii town ya Nairobi. Ndio William Ruto aheshimu Raila Odinga lazima tufunge biashara hii town," alisema.