Quincy Timberlake akiri shtaka la kuua mwanawe bila kukusudia

Mahakama imeratibiwa kumhukumu Timberlake mnamo September 29 mwaka huu.

Muhtasari

• Awali Timberlake alikuwa ameambia mamlaka kwamba mtoto wake alifariki baada ya kuanguka chini kwenye ngazi na kupata majeraha yaliyosababisha kifo chake.

Esther Arunga na mumewe Quincy Timberlake. Picha/MAKTABA
Esther Arunga na mumewe Quincy Timberlake. Picha/MAKTABA

Quincy Timberlake bwanake aliyekuwa mwanahabari Esther Arunga amekiri kumuua mwanawe wa kiume.

Quincy ambaye wakati mmoja alikuwa mgombea urais nchini Kenya, amekiri kosa la mauaji ya kutokusudia  ya mtoto wake wa miaka mitatu, Sinclair, nyumbani kwake mtaa wa Kallangur kaskazini mwa mji wa Brisbane, Australia.

Timberlake, ambaye alikuwa amepangiwa kujibu mashtaka ya mauaji ya kukusudia katika Mahakama ya Brisbane wiki hii, siku ya Jumanne alishangaza mahakama kwa kukubali kwa urahisi shtaka dogo la kuua bila kukusudia.

Upande wa mashtaka ulikubali ombi hili na baadaye akatupilia mbali shtaka la mauaji.

Awali Timberlake alikuwa ameambia mamlaka kwamba mtoto wake alifariki baada ya kuanguka chini kwenye ngazi na kupata majeraha yaliyosababisha kifo chake.

Licha ya juhudi za wahudumu wa afya, Sinclair alifariki muda mfupi baada ya tukio la 2014. Madai ya Timberlake hata hivyo yalikanwa na mkewe , Esther Arunga aliyeambia polisi kwamba mumewe alimuua mvulana huyo mdogo kwa kumpiga ngumi tumboni na kumtupa ukutani.

Alipatikana na hatia ya kushiriki katika mauaji ya mwanawe kwa kujaribu kuficha ukweli kuhusu matukio yaliyosababisha kifo cha Sinclair. 

Mahakama imeratibiwa kumhukumu Timberlake  mnamo September 29 mwaka huu. Hukumu ya kuua bila kukusudia ni nafuu kidogo ikilinganishwa na hukumu ya hatia ya mauji ya kukusudia.