DCI kuwasilisha mashtaka tisa dhidi ya Mackenzie na wenzake 95 ikiwemo mauaji

95 hao watakabiliwa na mashtaka ya kuua bila kukusudia na kushambulia na kusababisha madhara ya mwili na mauaji.

Muhtasari

• Januari 9, serikali ilipewa siku 14 kuwasilisha mashtaka dhidi ya Mackenzie na washukiwa wengine 17 wanaohusishwa na mauaji ya Shakahola.

paul mackenzie na mkewe Rhoda Maweu
paul mackenzie na mkewe Rhoda Maweu

Mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie na wafuasi wake 95 watashtakiwa kwa jumla ya makosa tisa, Ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) imethibitisha.

Kulingana na taarifa ya ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya umma siku ya Jumanne washukiwa hao akiwemo mshukiwa mkuu Mchungaji Paul Mackenzie, watawasilishwa mbele ya Mahakama Kuu.

Miongoni mwa mashtaka mengine 95 hao watakabiliwa na mashtaka ya  kuua bila kukusudia na kushambulia na kusababisha madhara ya mwili na mauaji.

Pia watashtakiwa kwa kujihusisha na uhalifu uliopangwa, kueneza itikadi kali na kutekeleza kitendo cha kigaidi chini ya Sheria ya Kuzuia vitendo vya Ugaidi, 2012 na Sheria ya Kuzuia Uhalifu uliopangwa, 2010.

Mchungaji Paul Mackenzie
Mchungaji Paul Mackenzie Mchungaji Paul Mackenzie

Chini ya makosa katika Sheria ya Mtoto, 200l; Sheria ya Kuzuia Mateso dhidi ya watoto, 2017 na Sheria ya Elimu ya Msingi, 2013, watuhumiwa watafunguliwa mashtaka ya kuwatesa watoto, kuwafanyia ukatili na kukiuka haki za watoto kupata elimu.

Mnamo Januari 9, serikali ilipewa siku 14 kuwasilisha mashtaka dhidi ya Mackenzie na washukiwa wengine 17 wanaohusishwa na mauaji ya Shakahola.

Zaidi ya miili 420  ya wafuasi wa dhehebu la Good News International ilifukuliwa kutoka msitu wa Shahola kuanzia Novemba 21, 2023, ambapo wafuasi hao waliombwa wafunge hadi wafe ili ‘kumlaki Yesu’.