Familia ya mwanafunzi aliyeuawa kinyama yatambua kichwa chake

Familia iliweaweza kutambua kichwa hicho kutokana na umbo la paji la uso wake, nywele na mpangilio wa meno.

Muhtasari

• Familia hiyo ilikuwa imetambua blauzi ambayo ilipatikana ikiwa imefungwa kichwani wakati kilipatikana.

Rita Waeni Muendo.
Rita Waeni Muendo.
Image: HISANI

Familia ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu aliyeuawa Rita Waeni imethibitisha kuwa kichwa kilichokatwa na kupatikana katika bwawa la Kiambaa, Kiambu, siku ya Jumapili ni mwanafunzi huyo.

Waliweza kutambua kichwa hicho kutokana na umbo la paji la uso wake, nywele na mpangilio wa meno.

Hatua hiyo iliwapa wanapatholojia wakiongozwa na mwanapatholojia mkuu wa serikali Johansen Oduor fursa kufanyia kichwa hicho uchunguzi kama sehemu ya juhudi za kubaini jinsi alifariki mnamo Januari 13 katika jumba moja eneo la Roysambu, Nairobi.

Zoezi hilo lilifanywa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City kufuatia lile la awali lililokuwa limefanywa kwenye sehemu nyingine za mwili.

Familia hiyo ilikuwa imetambua blauzi ambayo ilipatikana ikiwa imefungwa kichwani wakati kilipatikana.

Maafisa wa upelelezi wanashuku mauaji ya Waeni yalikuwa sehemu ya shughuli za ushirikina zinazoendelea nchini.

"Inaonekana kama ibada ambayo nadhani ilichochewa na imani kama ya kidini," afisa mmoja anayefahamu suala hilo alisema.

Kikosi cha uchunguzi kinataka kubaini kama kuna mauaji zaidi kama yale ya Waeni.

Mwili wa Waeni uliokuwa umekatwakatwa ulipatikana katika ghorofa moja eneo la TRM, Kasarani lakini kichwa chake hakikuwepo.

Kichwa hicho kilipatikana baadaye kikiwa kimefungwa kwa blauzi ya kike ya zambarau na kisha kuwekwa kwenye begi la kijani kibichi lenye jiwe ndani yake.