Nilimuua mtoto wangu kutokana na msongo wa mawazo, mama aiambia mahakama

Barbara Mutenyo alisimulia mahakama jinsi alivyomuua mwanawe mchana na kuufunga mwili wake kwenye gunia kabla ya kuutupa kisimani.

Muhtasari

• Mahakama ilisema kuwa baada ya kutekeleza mauaji hayo, mama huyo kijana alienda mafichoni kwa siku tatu ili kukwepa kukamatwa.

Msichana wa miaka 18 raia wa Uganda Babra Mutenyo katika Mahakama Kuu ya Eldoret jana wakati wa utetezi wake kuhusiana na mauaji ya mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miezi sita mwaka jana. Picha: JESSICAH NYABOKE
Msichana wa miaka 18 raia wa Uganda Babra Mutenyo katika Mahakama Kuu ya Eldoret jana wakati wa utetezi wake kuhusiana na mauaji ya mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miezi sita mwaka jana. Picha: JESSICAH NYABOKE

Mwanamke wa Uganda mwenye umri wa miaka 18 aliishangaza mahakama ya Eldoret baada ya kukiri kumuua mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miezi sita Oktoba mwaka jana.

Alitaka kujikomboa kutoka kwa mzigo wa kumtunza.

Barbara Mutenyo alisimulia mahakama jinsi alivyomuua mwanawe mchana na kuufunga mwili wake kwenye gunia kabla ya kuutupa kisimani.

"Ni kweli nilimuua mwanangu, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miezi sita, nilifunga mwili wake kwenye gunia na kisha kuutupa kisimani kwa vile sikuweza kumlea mtoto peke yangu," aliiambia mahakama.

Mshitakiwa huyo ambaye alionekana kuchanganyikiwa kizimbani, alidai kuwa kabla ya kutenda kosa hilo alipatwa na msongo wa mawazo, kutelekezwa na kuishi kwa hofu.

Mahakama ilisema kuwa baada ya kutekeleza mauaji hayo, mama huyo kijana alienda mafichoni kwa siku tatu ili kukwepa kukamatwa na polisi waliokuwa wakimtafuta baada ya kuarifiwa kuhusu tukio hilo na wakazi.

Baadaye aliibuka na kuelekea katika kituo cha polisi kilichokuwa karibu ambapo alikiri kutoweka baada ya kumuua mwanawe.

Polisi walimzuilia kwenye seli kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu shtaka la mauaji.

Mutenyo alijitetea mbele ya Hakimu Reuben Nyakundi katika kesi ambapo anashtakiwa kwa kumuua mwanawe, Junior Nesero Butsetse.

Inasemekana alitenda kosa hilo mnamo Oktoba 28, 2023 katika eneo la Kabogo katika kaunti ndogo ya Kapseret, kaunti ya Uasin Gishu.

Anawakilishwa na wakili Robert Makori huku upande wa mashtaka ukiongozwa na Mark Mugun.

Akijitetea kupitia kwa wakili wake, Mutenyo aliiomba mahakama kumpa adhabu ya kutozuiliwa endapo atapatikana na hatia ili kumwezesha kupata matibabu kutokana na kiwewe alichopitia baada ya tukio hilo baya.

Kwa mujibu wa wakili wake, mshtakiwa anahitaji urekebishaji, usaidizi wa kisaikolojia na kijamii na ushauri nasaha  ili aweze kujisimamia mwenyewe, kwa kuzingatia mazingira ambayo yalimsukuma kutenda kosa linalodaiwa.

Kesi hiyo itatajwa Aprili 18.