Jamaa afungwa miezi 6 kwa kumpiga mkewe aliyempakulia chakula na kuenda kulala

Hakimu aliamuru alipe faini ya Sh20,000 au akae jela miezi sita.

Muhtasari

• Joseph Kaniaru alishtakiwa kwa kumshambulia mkewe kwa ngumi na mateke punde baada ya kumpakulia chakula na kuenda kulala.

•Mshtakiwa alikubali mashtaka alipofikishwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Kibera William Tulei.

Joseph Kaniaru mahakamani Ijumaa
Joseph Kaniaru mahakamani Ijumaa
Image: CLAUSE MASIKA

Mwanamume mmoja alifikishwa kortini kwa kumshambulia mkewe kwa ngumi na mateke punde baada ya kumpakulia chakula na kuenda kulala.

Hakuna sababu nyingine nzito iliyotolewa mahakamani kwa nini mshtakiwa alichukua hatua hiyo.

 Joseph Kaniaru alikubali mashtaka alipofikishwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Kibera William Tulei Ijumaa.

Karatasi ya mashtaka iliyosomwa kortini inasema kwamba alitenda kosa hilo mnamo Julai 4, 2022 katika nyumba yao ya kupanga iliyo eneo la Kangemi, Nairobi.

Kulingana na upande wa mashtaka, mshtakiwa alizua ugomvi na mkewe, Teresia Wangari, dakika chache baada ya kumpa chakula alichokuwa ametayarisha.

Mahakama ilisema kuwa, mke huyo alienda kulala ili kupumzika kabla ya mshtakiwa kumnyakua kutoka kwa kitanda alichokuwa amelalia na kumshambulia kwa mateke na makofi yaliyomjeruhi jicho la kushoto na taya ya chini.

Mahakama ilisikia kwamba meno ya mlalamishi yalilegea ke kwenye taya ya chini na kuamua kuripoti kisa hicho kwa polisi, ambao baadaye walimkamata mshtakiwa.

Mshtakiwa alijieleza kuwa yeye ni mtu wa familia na akaomba mahakama imsamehe.

Hakimu aliamuru alipe faini ya Sh20,000 au akae jela miezi sita.