Kwa nini Tanzania inafanya vizuri kimuziki kuliko Kenya?

Mwandishi wetu alizamia suala hili na hapa ameibuka na majibu yaliyofanya Tanzania kuipiku Kenya kimuziki.

Muhtasari

• Kwa muda mrefu, Nchini Kenya kumekuwa na mjadala usiokuwa na mwisho kuhusu ni kipi kilitokea mpaka Tanzania wakatupiku kimuziki.

• Katika makala haya, tunajaribu kuangazia baadhi ya mambo na vitu ambavyo vinaweza kuwa vimechangia katika ukuaji wa kasi wa sanaa ya Tanzania.

Image: Shutterstock

Wikendi iliyopita, msanii Ommy Dimpoz alikuwa anazindua albamu yake ya kwanza kabisa tangu aanze muziki.

Kilichovutia wengi haswa wadau wa Sanaa ya muziki katika ukanda wa Afrika mashariki ni kitendo cha rais mstaafu Jakaya Kikwete kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa albamu hiyo.

Nchini Kenya, gumzo kubwa lilikuwa kuhusu jinsi ambavyo viongozi wa kisiasa nchini Tanzania wanawahendo na kuwapa sapoti wasanii wao, kinyume na humu nchini.Wengi walihisi kuwa viongozi wa kisiasa kuunga mkono juhudi za wasanii nchini Tanzania zimechangia kwa namna kubwa ukuaji wa Sanaa yao ya muziki ambayo sasa Bongo Fleva ndio gumzo la mjini na vijijini si tu Tanzania bali hata humu kwetu.

Kando na viongozi wa kisiasa kuenda bega kwa bega na wasanii katika kuwaonesha kuwa kazi yao ina mchango wa aina yake kwa jamii, pia tunaangali baadhi ya sababu zinazofanya Sanaa ya Tanzania kuwa bora kuliko Sanaa ya Kenya.

Viongozi kuunga mkono juhudi za wasanii

Kama tulivyoelezea hapo juu, nchini Tanzania viongozi wanawakubali sana wasanii wao na ndio maana wanatokea katika hafla zao kama za uzinduzi wa albamu na maonyesho mengine.

Kando na Kikwete kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa albamu ya Ommy Dimpoz, itakumbukwa mapema mwaka huu wakati msanii Diamond Platnumz alizindua EP yake ya FOA, wimbo wa ‘Nawaza’ ulitamba mpaka bungeni ambapo spika Tulia Ackson aliufagilia kwa kusema kuwa ndio wimbo wake penda.

Sasa unajiuliza ni kwa nini asilimia kubwa ya wasanii wa Tanzania wamemtungia wimbo rais Samia Hassan? Nadhani utakuwa tayari una jibu.

Nchini Kenya, ni adimu sana kumpata mwanasiasa akimpa sapoti ya njia yoyote ile au hata kutokea kwenye tamasha kwa kuonesha kudhamini kwake kazi za Sanaa ya wasanii wetu.

Wengi wanahisi hii ndio sababu muziki wa Kenya kwa kiasi kikubwa umedidimia.

 Wasanii kuwa na mameneja katika kazi zao za muziki

Jambo lingine ambalo limeleta ufanisi mkubwa katika Sanaa ya Tanzania ni hatua ya wqasanii wengi kukumbatia mfumo wa kuwa na mameneja wa kuendesha na kuratibu kazi zao za kimuziki.

Wasanii walitambua kuwa si kazi rahisi kufanya muziki na wakati huo huo kuwa katika soko la muziki kuzizukuma kazi zako, kwa sababu siku hizi muziki ni biashara! Msanii anapokuwa anajishughulisha kuandika ngoma nzuri studioni, huku nje meneja wake anahangaika kumtafutia mahojiano na kuusukuma muziki wake ili kuingiza pesa zaidi.

Hili ni kinyume na Sanaa ya Kenya ambapo wasanii wengi wanachipuka na kudidimia baada ya muda mfupi kutokana na kutojua jinsi ya kufanya muziki wa kibiashara – jambo ambalo ukiwa na meneja ni rahisi sana kutusua.

Wengi wa wasanii wa Kenya hawana uongozi katika kazi zao za kimuziki na hivyo huishia kujisikiliza tu kwenye simu zao kwani muziki wao haiendi mbali zaidi ya studio tu na baadhi ya marafiki.

Huduma nafuu za kimtandao

Mwaka jana, kampuni ya Cable.co.uk ilitoa ripoti kuwa huduma za intaneti nchini Kenya zipo ghali zaidi kuliko mataifa jirani katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Ripoti hiyo ilisema Tanzania wana huduma za intaneti za bei nafuu zaidi kuliko Kenya na Tanzania.

Hili pia linaweza kuwa moja ya sababu zinazofanya Sanaa ya Tanzania kua kwa kasi kutokana na dhana kwamba wengi wa wananchi wake wana uwezo wa kumudu huduma za mitandaoni, na hivyo kuifanya iwe rahisi kuzifikia kazi za Sanaa za wasanii wao na kuwapa umaarufu mkubwa – umaarufu ambao kwa kiasi kikubwa huoanishwa na mapato kwa sababu siku hizi faida nyingi za muziki hutokana na kufuatiliwa kwenye mitandao ya kijamii.

Idadi ya watu

Hivi majuzi, Tanzania walifanya sense ambapo matokeo yake yalionesha kuwa taifa hilo lina idadi ya watu milioni 61 na ushee.

Hii ni idadi kubwa ikilinganishwa na Kenya ambayo tuko watu milioni 50, kutokana na ripoti ya sense iliyofanywa miaka 3 iliyopita.

Wadau katika Sanaa ya muziki wakitolea mfano wa taifa la Nigeria, wanasema kuwa wingi wa watu unaoanishwa moja kwa moja na ufanisi katika kusambazwa kwa kazi za sana.

Kwa mfano taifa la Nigeria limetawala muziki wa Afropop kutokana na wingi wa watu huko ambao wanachangia katika kuupakua muziki huo na hivyo kufanya takwimu za kazi ya msanii kuenda juu.

Tanzania wanajivunia idadi kubwa ya watu ambao ni watumizi wa mitandao ya kijamii, hivyo basi ni rahisi kwa kazi ya msanii inapowekwa kwenye majukwaa ya kidijitali ya kupakua miziki, wengi hupata kuzifikia kupitia ‘streaming’

Idadi ya watu ikijumuishwa na unafuu wa huduma za kimtandao, unapata kwamba Tanzania inaipiga Kenya kumbo katika Sanaa na hivyo kupata mafanikio makubwa kutokana na Sanaa kuliko Kenya.

Wanasema wengi ndio hutoa kauli ya mwisho, na kweli Tanzania kutokana na wingi wao wanatawala muziki na wamepenya mpaka vitongojini Kenya.

Utunzi mzuri wa mashairi

Kama kuna kitu ambacho wasanii wa Bongo wengi wamekinata viganjani mwao basi ni weledi katika kutunga mashairi yenye vina na mtiririko kishairi.

Wengi wa wasanii hao wanatumia lugha ya Kiswahili kiufasaha zaidi katika kujieleza ,haswa ikija ni nyimbo za kiharakati kutokakwa marapa kama vile Roma Mkatoliki, Nay wa Mitego, Professor Jay, Kala Jeremiah miongoni mwa wengine.

Mtiririko wao wa mawazo katika miziki na kuwekeza katika biti nzuri kwenye studio za maana vimefanya muziki wao kuwa pendwa miongoni mwa watu wengi katika ukanda huu, tofauti na wasanii wetu wa Kenya ambao hawana mtindo maalumu wa kukumbatia kuwa ndio asilia wa sanaa ya Kenya.

Nchini Kenya kuna uhaba wa studio nzuri za kurekodi muziki unaoweza kutusua kimataifa kama Tanzania, kwa maana hiyo unapata muziki wetu unaishia tu kwenye vijiwe na mitaa.

Picha ya msanii Nyashinksi wa Kenya na Diamond Platnumz wa Tanzania
Picha ya msanii Nyashinksi wa Kenya na Diamond Platnumz wa Tanzania
Image: YouTube//Shanz On The Move