Mlo wa wali unaoaminika kuongeza 'nguvu za kufanya mapenzi'

Mlo huo unaaminika sana kuwa na uwezo wa kuongeza hamu ya kufanya mapenzi.

Muhtasari

•Huanza kwa kupika nyama (mchanganyiko wa nyama ya kondoo na nyama ya ng'ombe) kabla ya kuongeza karoti nyeupe na njano, vitunguu, wali, maji na viungo.

•Kulingana na Sagdiyev, wanaume wengine hutania kwamba neno plov kwa kweli linamaanisha uasherati kabla ya ndoa.

Image: BBC

Plov, mlo wa kitaifa unaopendwa nchini Uzbekistan, unaaminika sana kuwa na uwezo wa kuongeza hamu ya kufanya mapenzi. Kwa hivyo, kawaida huliwa siku ya Alhamisi. Alhamisi inachukuliwa kuwa siku mahsusi kwa wanawake kupata mimba.

Mlo huu unaoitwa plov, mchanganyiko wa mchele, mboga mboga, nyama na viungo, ni maarufu katika nchi zote za ukanda huo, lakini una uhusiano mkubwa na Uzbekistan.

Watu wa Uzbekistan hula plov angalau mara moja kwa wiki. Ni mlo wa kitaifa wa nchi na sehemu ya sherehe za familia.

Plov pia huliwa wakati wa kuzaliwa, harusi na mazishi, na pia kama njia ya kuwaheshimu Waislamu wanaorudi kutoka kuhiji.

Kulingana na hadithi, chakula hicho kiligunduliwa na Alexander the Great. Aliamuru kutayarishwa kwa chakula cha kutosha kuendeleza jeshi lake wakati wa vita huko Asia ya Kati.

"Hatuna rekodi za kihistoria za kuthibitisha hilo, lakini tunajua kwamba plov ilianza kujulikana sana hapa kufikia karne ya tisa na kumi," alisema kiongozi wa watalii wa Uzbekistan Nilufer Nuriddinova, mpenda historia ya chakula.

Mpunga umekuwa zao kuu katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 1,000.Hugharimu nguvu kubwa ya kimwili ili kuikuza. Pia unahitaji bidii kwa ajili ya uvunaji na ufugaji. Kwa hivyo Plov ingekuwa chakula bora cha kalori nyingi, chenye virutubishi kwa jamii ya wakulima.

Plov inachukuliwa kuwa sehemu muhimu ya mila ya upishi ya nchi hiyo hivi karibuni iliwekwa kwenye orodha ya UNESCO ya Turathi Zisizoguswa za Binadamu. Nuriddinova alisema, "Plov ni zaidi ya mlo. Unajenga uhusiano wa kijamii, unahimiza urafiki na kuunganisha nchi yetu.

Maisha nchini Uzbekistan hayawezekani bila plov

Image: BBC

Akifafanua neno hilo kama sehemu muhimu ya lugha ya Uzbekistan, alisema, “Pia linasikika katika misemo mingi ya kila siku. Kama, ikiwa ulikuwa na siku ya mwisho ya kuishi duniani, itumie kula plov. Ina maana unaweza kufa kwa furaha. Maisha nchini Uzbekistan hayawezekani bila plov.”

Zaidi ya aina 100 za plov zinapatikana nchini Uzbekistan. Mapishi hutofautiana kulingana na kanda na msimu, lakini kila tofauti inajumuisha viungo muhimu, herufi ambazo huupatia mlo jina lake kamili, osh palov. Hizi ni pamoja na o kwa ob (maji kwa lugha ya Kiajemi), sh kwa sholi (mchele), p kwa pioz (vitunguu), a kwa ayoz (karoti), l kwa lamh (nyama), o kwa olio (mafuta) na vat ( chumvi).

Mgahawa maarufu wa plov nchini, Besh Quezon (pia unajulikana kama Kituo cha Plov cha Asia ya Kati) uko Yunusabad, mji mkuu wa Tashkent.

Unachukuliwa kuwa moja ya miGahawa mikubwa zaidi ya plov katika Asia ya Kati. Bash Quezon hutoa plov kwa wateja 5,000 hadi 8,000 kila siku.

Image: BBC

Mchakato wa kupikia plov hufuata taratibu hizi. Huanza kwa kupika nyama (mchanganyiko wa nyama ya kondoo na nyama ya ng'ombe) kabla ya kuongeza karoti nyeupe na njano, vitunguu, wali, maji na viungo.

Sagdiyev hasa hutumia mchanganyiko wa chumvi, pilipili, manjano na binzari nyembemba. Haya yote yalikuja Uzbekistan kwanza kutoka India.

Hupikwa kwa saa nne kabla ya kuongeza mbaazi na zabibu kavu.

Alhamisi na Jumapili zinachukuliwa kuwa siku maarufu zaidi za kupika na kula plov huko Uzbekistan.

Nuriddinova alisema, "Katika nyakati za zamani, watu kutoka maeneo ya vijijini waliweza kwenda kwenye soko la jiji mara mbili tu kwa wiki kuuza bidhaa zao. Kwa hiyo walikuwa na pesa nyingi zaidi mifukoni mwao Alhamisi na Jumapili. Kwa sababu hiyo waliweza kununua bidhaa zote zinazohitajika kwa ajili ya mapishi ya plov.”

Sagdiyev anasema kuwa moja ya sababu kwa nini plov huliwa sana siku ya Alhamisi ni kwa sababu inaaminika kuwa na nguvu za kuongeza hamu ya kujamiiana. Inachukuliwa kuwa inafaa kabisa kuliwa siku za wanawake kushika mimba.

Kulingana na yeye, wanaume wengine hutania kwamba neno plov kwa kweli linamaanisha uasherati kabla ya ndoa.

Mafuta yanayopatikana chini ya sufuria hutumiwa kama Viagra ya asili. Wapishi wengi huhifadhi nyama bora Alhamisi ili kuwapa wateja wa kiume nguvu za ziada za kujamiiana.

Mila ya kutunga mimba siku ya Alhamisi inahusishwa na imani kali za Kiislamu nchini humo. Sagdiyev alisema, "Nabii Mohammad inaaminika kuwa alitungwa mimba siku ya Alhamisi.

Kwa hiyo ukitaka mtoto wako awe na akili, mtiifu, mwenye baraka kutoka kwa Mungu na kuwa na moyo wa ukarimu wa kupokea neema ya Mungu, Alhamisi ni siku nzuri kwake, lakini kabla ya hapo ni muhimu kula plov ya kutosha."