Chebukati akutana na makamishna 'waasi' mara ya kwanza tangu kutofautiana

Mwenyekiti wa IEBC aliongoza mkutano na wagombeaji kutoka maeneo ambayo uchaguzi uliahirishwa.

Muhtasari

•Waliokuwa Bomas ni pamoja na makamu mwenyekiti Juliana Cherera na makamishna Abdi Guliye, Boya Molu, Justus Nyang’aya, Irene Masit na Francis Wanderi.

•Jumatatu wiki iliyopita Cherera, Nyang'anya, Masit na Wanderi walijitenga na matokeo ya urais hata kabla ya Chebukati kuyatangaza.

Makamishna wote saba wa IEBC wamekutana katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Bomas of Kenya Jumatatu asubuhi.
Image: ENOS TECHE

Makamishna wote saba wa IEBC wamekutana katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Bomas of Kenya Jumatatu asubuhi.

Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati aliongoza mkutano na wagombeaji kutoka maeneo ambayo uchaguzi uliahirishwa.

Uchaguzi wa ugavana wa Kakamega na Mombasa ulikuwa ufanyike Agosti 23 lakini Chebukati wiki jana alisema umeahirishwa kwa muda usiojulikana.

Uchaguzi wa wabunge katika maeneo ya Rongai, Kitui vijijini, Kacheliba na Pokot Kusini pia ulikatizwa.

Jumatatu asubuhi, bosi huyo wa IEBC alisema uchaguzi katika maeneo hayo sasa utafanyika mnamo Agosti 29.

Waliokuwa Bomas ni pamoja na makamu mwenyekiti Juliana Cherera na makamishna Abdi Guliye, Boya Molu, Justus Nyang’aya, Irene Masit na Francis Wanderi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Chebukati kukutana na makamishna wote baada ya Cherera kuwaongoza wenzake watatu -Nyang'anya, Masit na Wanderi kukataa matokeo ya urais.

Jumatatu wiki iliyopita Cherera, Nyang'anya, Masit na Wanderi walijitenga na matokeo ya urais hata kabla ya Chebukati kuyatangaza.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari wiki jana, wanne hao walitoa sababu nne za kujitenga na matokeo yalioashiria kuwa William Ruto ndiye rais mteule.

Cherera alisema hesabu ya mwisho ya matokeo ya kura za urais zilizopigwa Agosti 9 haikuingiana na  ilipinga mantiki.

Naibu mwenyekiti huyowa  IEBC pia aliibua madai kuwa matokeo ya mwisho ya urais katika fomu 34C hayakuonyesha idadi ya watu ambao walipiga kura, kura halali zilizopigwa na kura ambazo zilikataliwa.

Alisema tume ilikosa uwazi kuhusu jinsi mchakato wa mwisho wa kujumlisha ulikuwa ukiendelea.

Pia walisema walikataa kumiliki matokeo kwa sababu matokeo yanatangaza idadi ya wapiga kura waliojiandikisha, kura zilizopigwa na idadi ya kura zilizokataliwa.

Walihoji jinsi mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alivyosema kwamba Raila alipata asilimia 25 ya kura katika kaunti 34 huku Ruto akipata asilimia 25 katika kaunti 39 ilhali kuna kaunti 47 pekee nchini.

Maafisa hao walisema sababu zilizotajwa hapo juu ziliarifu uamuzi wao wa kupinga matokeo.