Mwenye nyumba akamatwa baada ya kuteketeza nyumba ya mpangaji wake

Muhtasari
  • Mwenye nyumba akamatwa baada ya kuteketeza nyumba ya mpangaji wake
Pingu
Image: Radio Jambo

Familia moja huko Mumias, kaunti ya Kakamega, ililazimika kulala kwenye baridi kali baada ya mama mwenye nyumba kuteketeza nyumba yao, kwa sababu ya kutofautiana kuhusu malipo ya kodi.

Kulingana na ripoti ya polisi, Caroline Mukolwe, mmiliki wa nyumba hiyo alimwendea mpangaji huyo Alhamisi jioni akidai kodi ya nyumba ya Sh800.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai George Kinoti alisema mpangaji, ambaye hakuweza kuongeza pesa zote mara moja, alimpa mama mwenye nyumba Sh400 akiahidi kulipa salio ndani ya siku chache.

"Lakini mama mwenye nyumba aliyeonekana kukosa subira ambaye hangesikia ombi lake lolote la kuomba muda zaidi wa kutafuta pesa iliyosalia, alikimbia kurudi nyumbani kwake na kurudi mbio akiwa ameshikilia chupa iliyojaa mafuta ya taa na kiberiti," Kinoti alisema katika taarifa yake kupitia Twitter siku ya Ijumaa.

"Aliingia ndani ya nyumba ya mpangaji, akamwaga matandiko na nguo zake kwa mafuta ya taa na kuwasha moto, na kufanya mali ya maskini kuwa majivu."

Mpangaji huyo mwenye umri wa miaka 40, Teresia Ayeng alilazimika kutazama bila msaada huku mali yake ya thamani ya takriban Sh47,000 ikiteketea kwa moto.

"...mama mwenye nyumba alipanda na kushuka eneo la moto kwa shangwe," polisi walisema.

Maafisa wa polisi huko Mumias walimkamata mshukiwa ambaye atafikishwa mahakamani kujibu uhalifu wake.