Wanafunzi 44, walimu wanne wajeruhiwa katika ajali ya barabarani Kisumu

Muhtasari
  • Wanafunzi 44, walimu wanne wajeruhiwa katika ajali ya barabarani Kisumu
  • Basi la shule lilihusika katika ajali hiyo eneo la Mamboleo kando ya barabara ya Kisumu Kakamega
Basi la shule lilihusika katika ajali hiyo eneo la Mamboleo kando ya barabara ya Kisumu Kakamega.
Image: FAITH MATETE

Ajali ya barabarani iliyohusisha basi la shule iliwaacha wanafunzi 44 na walimu wanne wa Shule ya upili ya Thur-Gem wamejeruhiwa Alhamisi jioni.

Basi la shule lilihusika katika ajali hiyo eneo la Mamboleo kando ya barabara ya Kisumu Kakamega.

Basi la shule lilikuwa linatoka eneo la Bukura likielekea shule ya Thur-Gem huko Nyakach lilipopata ajali.

Basi hilo, kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo, lilipoteza mwelekeo na kutua kwenye mtaro ndani ya eneo la Coptic.

Wanafunzi waliokuwa wakigugumia kwa maumivu na kupiga mayowe walisaidiwa na wenyeji waliowatoa nje ya gari.

Akizungumza na vyombo vya habari katika eneo la tukio, OCPD wa kati wa Kisumu Anthony Maina alisema jumla ya wanafunzi 44 walipanda basi hilo pamoja na walimu wanne.

Maina alisema majeruhi walikimbizwa katika hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga ambako wanaendelea na matibabu.