Mtoto shujaa atibua jaribio la ubakaji huku mtuhumiwa akishtakiwa

Muhtasari

• Mtoto huyo alizua vita vikali dhidi ya fisi huyo mla watu katika hali ya kujaribu kujinasua mpaka akamlemea Odongo na kuchana mbuga kuelekea nyumbani kwao

• Mwanaume huyo aliyetambulika kwa jina Peter Odongo alimvizia mtoto huyo alipokuwa akienda shuleni kwa baiskeli katika Kijiji cha Changinywa kaunti ya Makueni.

Mahakama
Mahakama
Image: HISANI

Mwanaume aliyejaribu kumbaka mtoto wa miaka 13 ashitakiwa

Mwanaume huyo aliyetambulika kwa jina Peter Odongo alimvizia mtoto huyo alipokuwa akienda shuleni kwa baiskeli katika Kijiji cha Changinywa kaunti ya Makueni.

Kwa ulafi wa fisi, Odongo alimvizia mtoto huyo na kumvuta kwa nyuma na kisha kumburura hadi kichakani kando ya barabara alipomjaribu kumtendea ukatili wa kingono.

Mtoto huyo alizua vita vikali dhidi ya fisi huyo mla watu katika hali ya kujaribu kujinasua mpaka akamlemea Odongo na kuchana mbuga kuelekea nyumbani kwao alipomtaarifu mamake ambaye kwa ghadhabu alimfikisha katika kituo cha afya cha Kibwezi kwa vipimo vya afya na baadae akaelekezwa kuandikisha taarifa kwa polisi dhidi madai ya kujaribu kubakwa kwa mwanae.

Polisi walipopata taarifa hizo moja kwa moja walianzisha msako dhidi ya Odongo ambaye baadae alikamatwa katika shamba lake na kufikishwa mahakamani Februari 1 ili kujibu mashtaka ya kujaribu kumbaka mtoto mdogo kinyume na kifungu cha tisa cha sheria ya makosa ya ubakaji cha katiba ya kenya ya mwaka 2010.

Hiki ni kisa kimoja miongoni mwa visa vingi tu vya unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji ambavyo katika miaka ya hivi karibuni vimekuwa vikiripotiwa nchini, huku waasiriwa wengi wakiwa ni wale wa jinsia ya kike.

Wapelelezi wa DCI wamewashauri wazazi kuwasindikiza wanao shuleni kupitia njia salama ili kuepuka vitendo vya kinyama kama hivi na pia wananchi wameshauriwa kupiga mara wanapoona visa hivi vikitendeka katika jamii.