Ruto aomba Kongo Msamaha kwa matamshi yake

Muhtasari

• Naibu rais William Ruto hatimaye amelazimika kuomba msamaha kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya matamshi yake kupokelewa kwa njia hasi

• Februari 15, Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nchini Kenya Bi. Francine Muyumba alidhihirisha wazi kutofurahishwa kwake na matamshi ya Ruto kwamba nchi ya Kongo haina ng’ombe

William Samoei Ruto
Image: Facebook

Naibu rais William Ruto hatimaye amelazimika kuomba msamaha kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya matamshi yake kwamba taifa hilo halina ng’ombe kuzua mtafaruku na tishio la kuhatarisha mahusiano ya kidiplomasia baina ya Kenya na DRC.

Ruto ambaye amekejeliwa mno na viongozi mbalimbali kutoka mataifa haya mawili kwa matamshi yake ya kiholela, ameomba msamaha ila amesisitiza kwamba matamshi yake yalinukuliwa vibaya kwa njia ambayo yeye hakuwa ameilenga.

Katika taarifa zilizotumwa kwa vyombo vya habari na mkurugenzi wa mawasiliano ya kampeni za William Ruto, Hussein Mohamed, Ruto anasisitiza kwamba matamshi yake yalikuwa ya kawaida tu na kutumia maneno fulani katika matamshi yake kulikuwa kunalenga kusisitiza tu ukubwa wa nafasi za kibiashara zilizopo nje ya nchi kwa wakulima kuuza bidhaa zao.

“Hotuba yangu haikuwa rasmi na matumizi yangu ya maneno fulani ilikuwa ni kutilia mkazo tu ukubwa wa fursa za masoko ya bidhaa zinazotokana na mifugo ili hadhira ya humu nchini ipate uelewa. Matamshi yangu hayakukusudia kokosea heshima kwa njia yoyote,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

Ruto amesikitika ni kwa jinsi gani maadui wake wa kisiasa waliyachukulia maneno hayo na kuanza kumpiga vita vya kisiasa na kusema kwamba ameliomba taifa la Kongo na wananchi wake msamaha kwa mkanganyiko uliotokana na matamshi yake.

“Nasikitika sana kutoelewana na mkanganyiko uliotokea kwa sababu ya matamshi yangu, na kuchukua fursa hii kuihakikishia DRC kwamba ninavutiwa na taifa hilo na nina heshima kubwa kwao,” Ruto alisema.

Februari 15, Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nchini Kenya Bi. Francine Muyumba alidhihirisha wazi kutofurahishwa kwake na matamshi ya Ruto kwamba nchi ya Kongo haina ng’ombe hata mmoja na kusema matamshi hayo ni ya kudhalilisha na kuwakosea watu wa Kongo heshima, jambo ambalo lilizua mijadala mikali mitandaoni, baadhi ya viongoni wakimshrutisha Ruto kutoa msamaha wa wazi kwa Kongo