Serikali inalenga kuokoa angalau shilingi bilioni 300- Ruto

Alisema ni makosa na sio endelevu kwamba serikali ililazimika kukopa fedha kwa ajili ya matumizi ya sasa.

Muhtasari
  • Bajeti iliyosomwa Aprili 7, 2022, na Waziri wa Hazina anayeondoka Ukur Yatani ilifikia jumla ya Sh3.3 trilion
RAIS WILLIAM RUTO
Image: EZEKIEL AMING'A

Rais William Ruto ameagiza Hazina ya Kitaifa kupunguza bajeti ya 2022/23 kwa Sh300 bilioni.

Alisema upunguzaji huo utasaidia serikali kuchangia juhudi za kuokoa taifa kwa kuweka matumizi ya kawaida chini ya mapato.

Alizungumza alipofungua rasmi bunge la 13 siku ya Alhamisi.

“Nimeiagiza Hazina ya Taifa kushirikiana na wizara kutafuta akiba ya Sh300 bilioni katika bajeti ya mwaka huu,” alisema.

Juhudi za kuweka akiba zitachukua miaka mitatu, ambayo itasababisha ufadhili wa kujitegemea wa matumizi ya kawaida.

"Mwaka ujao, tutaipunguza zaidi ili, kufikia mwaka wa tatu, tuwe na ziada ya bajeti," Ruto aliongeza.

Alisema ni makosa na sio endelevu kwamba serikali ililazimika kukopa fedha kwa ajili ya matumizi ya sasa.

"Mwaka huu pekee, tulipanga bajeti ya kukopa Sh900 bilioni ili kufadhili matumizi ya maendeleo na ya kawaida," alisema.

Bajeti iliyosomwa Aprili 7, 2022, na Waziri wa Hazina anayeondoka Ukur Yatani ilifikia jumla ya Sh3.3 trilioni.