Mwanaume apoteza wazazi kwenye mkasa wa jengo lililoporomoka Kiambu

Wawili hao walifariki baada ya kuporomokewa na jengo la ghorofa 5.

Muhtasari

• Waliporomokewa na jengo hilo la ghorofa 5 na kufa papo hapo.

• Fred Kamamu aliwapoteza wazazi wake wawili kwa siku moja kwenye mkasa huo uliotokea alfajiri ya Alhamisi.

Azishika picha za wazazi wake waliofaliki kutokana na kuporomokewa na jengo Ruaka, Kiambu.
facebook Azishika picha za wazazi wake waliofaliki kutokana na kuporomokewa na jengo Ruaka, Kiambu.
Image: Radio jambo//Andrew Kasuku

Wingu la simanzi na majonzi  lilitanda kwenye moyo Fred Kamau ambaye alipigwa na butwaa baada ya kupata habari za kuhuzunisha za kufa kwa wazazi wake siku moja kwa mkasa wa jengo kuporomoka.

Wazazi wake Peter Juthi mwenye umri wa miaka 72 na mamake Faith Wambui mwenye umri wa miaka 60 walifariki dunia baada ya kuporomokewa kwa jengo la ghorofa 5 eneo la Ruaka, Kiambu.

Kamau ameachwa akiomboleza wazazi wake kwa kushikilia picha ambazo zitakuwa zinamtonesha kidonda cha moyo wakati atakuwa akizitazama na kuwakumbuka wazazi wake.

Picha za Faith Wambui (60) na Peter Juthi (72).
Picha za Faith Wambui (60) na Peter Juthi (72).
Image: Andrew Kasuku

Kwenye mkasa huo ambao ulitokea asubuhi ya kuamkia Novemba 17, 2022 uliangukia makazi ya majirani waliokadilia hasara kubwa kutokana na jengo hilo.

Kwingineko wakaazi wameachwa na bumbuazi na kimako baada ya wanandoa wengine wawili kufariki. Mzee wa miaka 73 na mkewe mwenye umri wa miaka 52 waliipa dunia kisogo walipokuwa wamelala kwenye nyumba ya mabati karibu na eneo la ujenzi.

Kulingana na ripoti, watoto wao 3 hawakujeruhiwa kwani walikuwa wakiishi katika nyumba nyingine ndani ya boma hilo.

"Ninaishi katika jengo lililokaribu  na niliposikia kishindo, nilikimbilia nje. Kwa msaada wa wengine waliokuja tulichomoa vifusi lakini kwa bahati mbaya kaka yangu na mkewe walikuwa wamefariki,” alisema Antony Karomo ndugu wa marehemu.

Kulingana na ripoti manusura watatu walipelekwa hospitalini huku juhudi za kuwaokoa wengine zikiendelea.