Kenya yatoa taarifa kuhusu mkasa wa tetemeko la ardhi Uturuki

Uturuki ilikumbwa na tetemeko baya zaidi la ardhi mapema Jumatatu na kuua watu zaidi ya 2000.

Muhtasari

• Katibu wa kudumu katika kitengo cha masuala ya wanaoishi nje ya nchi alisema hakuna Mkenya aliyejeruhiwa au kufa katika mkasa huo.

Image: Getty Images

Katibu wa kudumu katika kitengo cha serikali cha kushughulikia masuala ya wanaoishi nje ya Kenya Roseline Njogu amedhibitisha kwamba hakuna taarifa yoyote kuhusu Mkenya kujeruhiwa au kuwa mmoja wa walioathirika la tetemeko baya Zaidi ya ardhi lililotokea nchini Uturuki na Syria usiku wa kuamkia Jumatatu.

Mtetemeko huo wa ardhi ulitajwa kuwa mbaya Zaidi katika siku za hivi karibuni kwenye taifa hilo la bara Asia. Taarifa zinasema kuwa Zaidi ya watu elfu mbili wameripotiwa kuaga huku Zaidi ya elfu 7 wakiwa tayari wameokolewa.

Njogu alitoa namba ya dharura kwa Wakenya wote wanaoweza kuwa kwenye mkasa huo Uturuki au kujua mtu yeyote mwenye ako huko ili kubaini usalama wake.

“Kufuatia tetemeko la ardhi la leo nchini Uturuki na N. Syria, @KenyaEmbAnkara inathibitisha hakuna taarifa za Mkenya yeyote aliyefariki au kujeruhiwa. Wakenya walioathiriwa na tetemeko hili la ardhi wanaweza kupiga simu kwa nambari ya simu ya ubalozi +90(538)502 0960, barua pepe diaspora@mfa.go.ke au tutumie DM kwa @Diaspora_KE cc @ForeignOfficeKE. Janga kama hilo tetemeko la ardhi ni la Türkiye na Syria. Rambirambi zetu za dhati kwako. Mawazo yetu, sala na upendo kwa familia zilizofiwa na matumaini ya kupona kwa waliojeruhiwa,” Njogu aliandika Twitter.

Uturuki na Syria zilikumbwa na janga la kibinadamu ambalo halijawahi kushuhudiwa baada ya kukumbwa na matetemeko makubwa mawili ya ardhi katika muda wa chini ya saa 12. Tetemeko la kwanza la kipimo cha 7.8 lilipiga eneo hilo mapema asubuhi ya Jumatatu, 6 Februari, wakati raia wasio na mashaka na wakimbizi wamelala.