CS Kindiki:Odero kushtakiwa kuhusiana na vifo vya wafuasi wake

Kindiki alisema kuwa watu zaidi ya 100 wametolewa walikojificha ili kurekodi taarifa.

Muhtasari

• Ezekiel Odero alikamatwa siku ya Alhamisi na kanisa lake a New Life Prayer Centre kufungwa.

KITHURE KINDIKI AKIWA MBELE YA KAMATI YA USAILI YA BUNGE LA KITAIFA
Image: EZEKIEL AMINGA

Waziri wa usalama na masuala ya ndani,Kithure Kindiki sasa amesema kuwa mhubiri Ezekiel Odero wa kanisa la New Life Prayer Centre atashtakiwa kwa kuhusiana na vifo vya wafuasi wake.

Katika chapisho kwenye ukurasa wake  wa Twitter, Kindiki alitoa ripoti ya kukamatwa kwa mhubiri huyo na kuongezea kuwa kanisa lake limefungwa.

"Umma unataarifiwa kuwa siku ya Alhamisi tarehe 27 Aprili 2023, Bw Ezekiel Odero Ombok ambaye ni kiongozi wa kanisa la New Life Prayer Centre eneo la Mavuenini,Kaunti ya Kilifi amekamtwa na atashtakiwa  kuhusiana na mauaji ya wingi ya wafuasi wake," alisema Kindiki.

Waziri huyo aliongezea kuwa watu 100 ambao walikuwa wamejificha katika majengo hayo wametolewa na watarekodi taarifa.

Ezekiel Odero alikamatwa mapema  siku ya Alhamisi na polisi katika Kaunti ya Malindi eneo la Mavueni na kanisa lake kufungwa.

Odero alishikwa baada ya sakata inayohusishwa na mhubiri Paul Mackenzie aliyekamatwa siku kadhaa zilizopita kwa madai ya kuwapa wafuasi wake mafunzo potovu ailiyofanya wafunge hadi kufa kwa matumaini ya kukutana na Yesu.

Miili ya watu 98 sasa imefukuliwa katika shamba linalohusiana naye huku DCI ikiendeleza uchunguzi ya jinsi watu zaidi ya 100 waliweza kufa na kuzikwa bila kujulikana.