Nimewahi sujudu katika kanisa na Pasta Ezekiel, miujiza yake ni kweli - Mbunge amtetea

“Kwa sasa naweza sema mambo yake ni halali kwa sababu nimeshuhudia, nimewahi hata kufika kanisani na kusujudu pale." - Mbunge huyo alisema.

Muhtasari

• Pia mbunge huyo alisema kuwa atashangaa sana iwapo Ezekiel atashtakiwa kwani mambo mengi ambayo ameyafanya ni ya kibinadamu.

• Matendo yake si ya mazingaombwe au yanayoenda nje ya dini. Kama ni ushauri anatoa ule wa kidini,” mbunge alimtetea.

Pasta Ezekiel akamatwa, mbunge wa Magarini amtetea vikali.
Pasta Ezekiel akamatwa, mbunge wa Magarini amtetea vikali.
Image: Twitter

Mbunge wa Magarini kaunti ya Kilifi Harrison Kombe ameibua mapya kuhusu sakata linaloendelea kushika moto la mchungaji Paul Mackenzie kufuatia vifo vyenye utata vya makumi wa waumini wa kanisa lake huko Shakahola.

Kulingana na mbunge huyo, mchungaji Ezekiel Odero ambaye ametiwa mbaroni mapeni Alhamisi kufuatia za ndani zinazomhusisha na vitendo vya kupotosha kama vile vya Mackenzie, hahusiki kwa njia yoyote katika upotoshaji.

Kombe akizunumza asubuhi ya Alhamisi kwenye runinga ya Citizen alisema kwamba Odero ni mshirika wa kaunti kwa muda mrefu ambapo anatoa ushirikiano katika kufadhili masomo ya baadhi ya watoto wasiojiweza pamoja pia na kujenga vituo vya masomo na afya.

“Kwa muhtasari nimewahi kukutana naye, ni mshirika wa serikali ya kaunti, kuna mambo kadha wa kadha ambayo anafanya. Ndani ya Magarini anajenga zahanati ambapo ni kwa upande wa afya anajali na pia ameweza kutoa misaada ya chakula. Ni jambo ambalo tunalifurahia.”

Mbunge huyo pia alimtetea vikali Odero kwamba hajawahi kumshuhudia akifanya vitendo vya kupotosha kwa wumini wake kwani hata yeye amewahi kuabudu katika kanisa lake huko Mavueni.

“Kuna watu wametoka katika eneo bunge langu na kwenda mpaka kanisa la Ezekiel kwa ajili ya maombi na kurudi wakiwa katika hali salama. Na pia kwa ufahamu, ni kwamba sasa hivi Ezekiel anajenga chuo cha madaktari katika eneo lake,” Kombe alisema.

“Kwa sasa naweza sema mambo yake ni halali kwa sababu nimeshuhudia, nimewahi hata kufika kanisani na kusujudu pale. Na kama ni miujiza kufanyika inafanyika hapo hapo unaona, si mambo ya kwamba inakwenda kufanyiwa gizani halafu unaletewa huyo mtu, hapana,” mbunge Kombe alisema.

Kombe alikiri kwamba endapo atafunguliwa mashtaka ya kutoa mafunzo ya kupotosha, binafsi atashangaa sana.

“Mimi binafsi nitashangaa sana kwa sababu yale yote ambayo ameyatenda ni ya kibinadamu, ni matendo ambayo si ya mazingaombwe au yanayoenda nje ya dini. Kama ni ushauri anatoa ule wa kidini,” mbunge alimtetea.