Didmus Barasa apinga kukamatwa kwa pasta Ezekiel

Kwa hivyo mbunge huyo alitoa maoni kwamba Mungu angetoa adhabu yake kwa watu kwa kumkamata pasta.

Muhtasari
  • Alifikishwa mahakamani siku ya Ijumaa, ambapo polisi walitaka kumweka kizuizini kwa siku 30 zaidi wakisubiri kukamilika kwa uchunguzi.
Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa
Image: MAKTABA

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa sasa anaikosoa serikali kwa kumkamata mwinjilisti Ezekiel Odero anayedaiwa kuwa na uhusiano na Paul Mackenzie na mauaji ya halaiki ya zaidi ya watu 100 huko Shakahola, Kaunti ya Kilifi.

Mbunge huyo kupitia kwenye mitandao ya kijamii Alhamisi alilaani kufungwa kwa Kituo cha Maombi na mhubiri wa Kanisa akisema vitendo vya ibada vya baadhi ya viongozi wa kidini havipaswi kutumiwa kuwadhulumu wengine.

Barasa aliwaita Mackenzie na Yesu wa Tongaren akiwataja kama wahalifu, na kuongeza kuwa wanapaswa kuwajibika tu badala ya kulaaniwa kwa jumla kwa dini nzima.

“Sidhani kama ilikuwa halali kwa polisi kumkamata Mchungaji Ezekiel Odero. Mhalifu mmoja ambaye alikuwa akiendesha ibada na mwingine akijiita Yesu wa Tongaren hawezi kuwa sababu na au matokeo ya kulaaniwa kwa kanisa,” aliandika.

Kwa hivyo mbunge huyo alitoa maoni kwamba Mungu angetoa adhabu yake kwa watu kwa kumkamata pasta.

"Mungu atatuadhibu vikali kwa hili...ninapinga vikali kitendo hiki," alisema.

Mchungaji Ezekiel alikamatwa siku ya Alhamisi, siku moja baada ya kuhojiwa kuhusu madai ya kuwa na uhusiano na Mackenzie, kiongozi wa madhehebu ambayo yamesababisha vifo vya takriban watu 109 nchini Kenya, pamoja na madai ya kufunzwa na waumini.

Alifikishwa mahakamani siku ya Ijumaa, ambapo polisi walitaka kumweka kizuizini kwa siku 30 zaidi wakisubiri kukamilika kwa uchunguzi.

Mbunge wa Magarini kaunti ya Kilifi Harrison Kombe aliibua mapya kuhusu sakata linaloendelea kushika moto la mchungaji Paul Mackenzie kufuatia vifo vyenye utata vya makumi wa waumini wa kanisa lake huko Shakahola.

Kulingana na mbunge huyo, mchungaji Ezekiel Odero ambaye alitiwa mbaroni mapema Alhamisi kufuatia za ndani zinazomhusisha na vitendo vya kupotosha kama vile vya Mackenzie, hahusiki kwa njia yoyote katika upotoshaji.

Kombe akizunumza asubuhi ya Alhamisi kwenye runinga ya Citizen alisema kwamba Odero ni mshirika wa kaunti kwa muda mrefu ambapo anatoa ushirikiano katika kufadhili masomo ya baadhi ya watoto wasiojiweza pamoja pia na kujenga vituo vya masomo na afya.

“Kwa muhtasari nimewahi kukutana naye, ni mshirika wa serikali ya kaunti, kuna mambo kadha wa kadha ambayo anafanya. Ndani ya Magarini anajenga zahanati ambapo ni kwa upande wa afya anajali na pia ameweza kutoa misaada ya chakula. Ni jambo ambalo tunalifurahia.”