Uteuzi wa Kenya kwanza ndio mwanzo wa ufisadi-Seneta Osotsi

Osotsi aliendelea kusema kuwa historia ya ufisadi ya mtu ni muhimu katika kubainisha uteuzi.

Muhtasari
  • Seneta huyo aliendelea kudai kuwa uteuzi unaofanywa na serikali haulengi kuwasilisha maswala ya kimsingi yanayoathiri wananchi bali wale walioteuliwa kulipwa.
Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi

Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi amedai kuwa uteuzi uliofanywa na serikali ya Kenya Kwanza unachochea ufisadi.

Katika mahojiano katika kipindi cha DayBreak cha runinga ya Citizen mnamo Jumatatu, Seneta huyo alitoa maoni kuwa baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusika katika sakata hiyo ya sukari wanafanya kazi kwa karibu na rais.

"Baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusika katika sakata hii ya sukari na hata KEMSA walikuwa wameketi nyuma yake," alisema Osotsi.

Seneta huyo aliendelea kudai kuwa uteuzi unaofanywa na serikali haulengi kuwasilisha maswala ya kimsingi yanayoathiri wananchi bali wale walioteuliwa kulipwa.

"Hawa watu hawapangiwi huko kwenda kufanya kazi na kutoa, wanateuliwa huko kwenda kufanya kazi na kupata," alisema.

Katika kueleza jinsi maafisa wanavyojipanga kupata pesa kupitia ufisadi, alitoa mfano wa wajumbe wa bodi ambao kulingana naye wanastahili kupata takriban Ksh.320,000 kwa mwaka lakini wakaishia kuchuma zaidi.

Alitaja utoaji wa zabuni na ajira kuwa ni maeneo ambayo kuna rushwa na kwamba wajumbe wa bodi huwatumia maafisa wa kiufundi ili kuwezesha rushwa.

Seneta huyo alimtaka rais kuangalia umahiri wa wafanyikazi anaowateua serikalini.

"Kwa yeye kuwa makini na vita dhidi ya rushwa, nadhani inaanza na ubora, uwezo, umahiri na tabia za watu wanaoteuliwa," alibainisha.

Osotsi aliendelea kusema kuwa historia ya ufisadi ya mtu ni muhimu katika kubainisha uteuzi.

Aliongeza kuwa mtu anayekabiliwa na kesi za ufisadi hapaswi kuzingatiwa kazi za serikali isipokuwa kesi hizo zimefutwa kortini.