Kawangware: Wafanyabiashara wadogo wadogo wazua fujo vibanda vyao kubomolewa

Wafanyabiashara hao wametaka kujua ni kwa nini chanzo chao cha mapato kiliharibiwa.

Muhtasari

• Polisi waliwatawanya wafanyibiashara hao kwa kutumia vitoza machozi.

• Usafiri wa umma umetatizika, hakuna magari yanayosafirisha watu, na yaliyopo yamepandisha nauli.

Wafanyabiashara waliwasha moto kando ya Barabara ya Naivasha wakipinga kubomolewa kwa Vibanda vyao.
Wafanyabiashara waliwasha moto kando ya Barabara ya Naivasha wakipinga kubomolewa kwa Vibanda vyao.
Image: TABNACHA ODUOR

Wafanyibiashara wa mtaa wa Kawangware siku ya Ijumaa waliandamana wakilalamikia kubomolewa kwa vibanda vyao kwenye Barabara ya Naivasha.

Waliwasha magurudumu barabarani, na kusababisha msongamano wa magari kwenye barabara ya Naivasha.

Wafanyabiashara hao wametaka kujua ni kwa nini chanzo chao cha mapato yao kiliharibiwa.

 Polisi waliwatawanya wafanyibiashara hao kwa kutumia vitoza machozi.

Usafiri wa umma umetatizika, hakuna magari yanayosafirisha watu, na yaliyopo yamepandisha nauli.

Polisi wakizima moto baada ya kuwatawanya waandamanaji Ijumaa Mei 26.
Polisi wakizima moto baada ya kuwatawanya waandamanaji Ijumaa Mei 26.
Image: TABNACHA ODUOR

Utulivu ulirejea polepole baada ya polisi kuingilia kati, baada ya kuwatawanya waandamanaji hao, polisi walionekana wakizima moto uliokuwa umewashwa na waandamanaji hao.

Haya yanajiri huku Wakenya wengi wakilalamikia hali ya juu ya maisha, na kuongezeka kwa bei za bidhaa muhimu.

Wakenya hawa wanahisi ni kama Rais William Ruto anawasahau wafanyibiashara wadogo kwa kuongeza ushuru wa bidhaa muhimu hivyo kuzifanya bei za bidhaa hizo kuongezeka.

Katika kampeni za Rais Ruto aliwaahidi wafanyi biashara wadogo kama mama mboga, waendesha boda boda kuwa atahakikisha hali ya maisha itakuwa nafuu.

Hivi majuzi bei ya Sukari imeongezeka maradufu licha ya kuwa na madai kuwa sukari hii ilikuwa na sumu.

Aidha wakenya wengi walionyesha kutoridhika kwao kwa ahadi ya Rais ya kupunguza bei ya unga wa Ugali hadi shilingi 150 huku wakiendelea kusuburi ili kupata unga huu wa bei hio.