Polisi wamtaka 'Nabii Yohana' kutoka Bungoma kujiwasilisha kituoni kwa usaili

Kooli alisema mhubiri huyo, ambaye ana wake 42 na watoto 289, anachunguzwa kwa madai ya mafundisho yenye utata.

Muhtasari

• Kooli alisema pia wamemualika  mmiliki wa kanisa linaloitwa Choma kufika mbele ya maafisa wa polisi.

• Kamanda wa polisi wa kaunti ya Bungoma Francis Kooli alisema mhubiri huyo atahojiwa kuhusu mahubiri ya kanisa lake.

Mhubiri Ronald Wanyama Nabii Yohana.
Mhubiri Ronald Wanyama Nabii Yohana.

Polisi huko Bungoma wamemuamrisha mhubiri Ronald Wanyama anayefahamika kama Nabii Yohana kufika mbele yao ili kuhojiwa.

Mhubiri Ronald Nakalila Wanyama, 'Nabii Yohana', 83 anatarajiwa kufika mbele ya Kamanda wa Polisi wa Bungoma siku ya Ijumaa, Juni 2.

 Kamanda wa polisi wa kaunti ya Bungoma Francis Kooli alisema mhubiri huyo atahojiwa kuhusu mahubiri ya kanisa lake.

"Kuna baadhi ya masuala tunataka kuelewa kutoka kwake," alisema Kooli.

 Alisema hawawezi  kuelewa ikiwa kanisa linafanya kazi kama kituo cha uponyaji au shirika la kidini.

Kooli alisema pia wamemualika  mmiliki wa kanisa linaloitwa Choma kufika mbele ya maafisa wa polisi.

 "Tunataka kumuamrisha hapa. Tunataka kujua jinsi zinavyoendeshwa,” alisema.

 Nabii Yohana anaongoza kanisa la Church  for All Nations lililoko Kanduyi, kaunti ya Bungoma, na amewahi kugonga vichwa vya habari, ikiwa ni pamoja na madai kwamba angezindua biblia yake na sarafu yake mpya.

Kooli alisema mhubiri huyo, ambaye ana wake 42 na watoto 289, anachunguzwa kwa madai ya mafundisho yenye utata.

Anafahamika sana kwa, miongoni mwa mambo mengine, Biblia yenye vitabu 93 ambayo inasemekana aliandika na ambayo anaitumia kuhubiri kwenye kanisa lake.

Kamanda huyo wa polisi pia alisema mhubiri huyo  alipanga amri zake, na kupunguza zile kumi na mbili za asili zilizotolewa na Musa kwenye Bibilia hadi 10.

Mhubiri huyo ni wa pili katika eneo hilo kuamrishwa kufika mbele ya polisi kwa muda usiozidi mwezi mmoja kwa ajili ya mafundisho yenye utata.

Polisi walikuwa wamemwita mhubiri anayeishi Bungoma Eliud Wekesa, maarufu kama Yesu wa Tongaren kwa uchunguzi ila aliachiliwa na mahakama.

 Polisi wanataka kujua kama taasisi hizo zimesajiliwa kwa mujibu wa sheria.