CS Ababu abatilisha uteuzi wa Azziad na wenzake kuwa wanachama wa Talanta Hela

Waziri alibatilisha uteuzi aliofanya kutokana na utata unaozingira uteuzi huo.

Muhtasari

• Katika notisi ya gazeti la serikali siku ya Ijumaa, Waziri huyo alibatilisha uteuzi aliofanya awali kufuatia mzozo uliowakumba wanachama wa baraza hilo.

Waziri wa maswala ya sanaa na michezo, Ababu Namwamba.
Waziri wa maswala ya sanaa na michezo, Ababu Namwamba.
Image: MAKTABA

Waziri wa maswala ya sanaa na michezo Ababu Namwamba amebatilisha uteuzi wa Carol Radul, Dennis Itumbi, Azziad Nasenya, Daniel Ndambuki na wengine katika baraza la Talanta Hela na kamati ya kiufundi.

Katika notisi ya gazeti la serikali siku ya Ijumaa, Waziri huyo alibatilisha uteuzi aliofanya awali kufuatia mzozo uliowakumba wanachama wa baraza hilo.

"Inajulishwa kwa taarifa ya jumla ya umma kwamba katibu wa baraza la mawaziri la mambo ya vijana na sanaa amefuta Notisi ya Gazeti namba 1649 ya 2023," notisi hiyo inasomeka kwa sehemu.

Waziri huyo wa maswala ya vijana na spoti aliwateua watu hao maarufu mwezi wa Februari mwaka huu licha ya utata uliozingira uteuzi huo.

Kamati hiyo ya wabunifu ilikuwa itimize, miongoni mwa majukumu mengine, kukusanya na kusambaza mirabaha kwa wabunifu wote, kupendekeza mifumo ya utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Uchumi wa Ubunifu, kusimamia Tuzo za Kitaifa za Ubunifu (Grammys za Kenya) na kuanzisha mfumo thabiti wa kuchuma mapato kwa sekta ya ubunifu, kupanua fursa za ajira na kusaidia ukuaji wa uchumi wa Kenya.

Ababu Namwamba akizungumza na kituo moja cha radio humu nchini alisema kuwa mpango huo wa Talanta Hela, uambao unafaa kuweka pesa kwenye mifuko ya wasanii na wanamichezo nchini, utazinduliwa hii leo, Ijumaa.

"Rais William Ruto atazindua talanta Hela rasmi hapo kesho, sekta hii ya michezo imetelekezwa kwa muda mrefu sasa na huu ndio muda mwafaka kuweza kushughulikia sekta hii kwa kuwa ina uwezo wakuwaajiri watu wengi,” alisema Ababu.