Mswada wa Fedha unaopendekezwa wapitishwa huku wabunge 81 wakiupinga

Mswada huo ulipingwa na wabunge 81.

Muhtasari

• Wabunge176 wamepiga kura kuunga mkono Mswada wa Fedha wa 2023,huku 81 wakipinga.

• Mswada huo sasa unasonga mbele kwa kamati ya Bunge zima ambapo wabunge watapata nafasi ya kusukuma marekebisho yao.

Wabunge wakati wa ufunguzi wa Bunge baada ya kufanyiwa ukarabati.
Wabunge wakati wa ufunguzi wa Bunge baada ya kufanyiwa ukarabati.
Image: MAKTABA

Wabunge wamepiga kura kuunga mkono Mswada wa Fedha wa 2023, na hivyo kupisha njia ya kuamuliwa kwake na kamati ya Bunge zima.

Baada ya mjadala mkali Bungeni Jumatano wa kujadili mapendekezo ya kodi, wabunge 176 walipiga kura ya kuidhinisha katika hatua ya pili ya kusomwa kwa mswada huo huku wabunge 81 kati ya 257 wakipinga.

Mswada huo sasa unasonga mbele kwa kamati ya Bunge zima ambapo wabunge watapata nafasi ya kusukuma marekebisho yao.

Kamati hiyo itazingatia Mswada huo kifungu baada ya kifungu na kupiga kura kwa kila kifungu kibinafsi.

Hivi ndivyo baadhi ya wabunge walivyopiga kura; Mbunge wa Bomet Mashariki Richard Yegon alipiga kura ya Ndiyo, Charles Onchoke (Bonchari) alipiga kura ya hapana, Raphael Wanjala (Budalangi) alipiga kura ya hapana, Patrick Kibagendi (Borabu) alipiga kura ya hapana, Jack Wamboka (Bumula) alipiga kura ya hapana, Komingoi Kibet Kirui (Bureti) alipiga kura ya ndiyo huku Korir Adams Kipsanai (Keiyo Kaskazini) alipiga kura ya ndiyo.

Kipkoech Gideon Kimaiyo (Keiyo Kusini) alipiga kura ya ndiyo, Beatrice Kemei (Kericho) alipiga kura ya ndiyo, John Njuguna Wanjiku (Kiambaa) alipiga kura ya ndiyo naye John Waithaka Machua (Kiambu) alipiga kura ya ndiyo.

Rais William Ruto na kinara wa Azimio Raila Odinga walikuwa wamewatahadharisha wambunge wa mirengo hizi mbili kwamba watakuwa wakifuatilia mjadala huo kwa karibu ili kuona ni njia gani wangeupigia kura Mswada huo.

Siku ya Jumanne, Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Fedha na Mipango iliwasilisha Mswada wa Fedha wa 2023 uliorekebishwa baada ya umma kutoa maoni yao.

Kulikuwa na upinzani kuhusu mapendekezo fulani katika Mswada huo, ambayo Wakenya waliyataja kuwa ya kuadhibu.

Mswada huo, unapendekeza miongoni mwa mambo mengine tozo wa nyumba ya bei nafuu, ongezeko la VAT kwa bidhaa za petroli, na ushuru mpya kwa bidhaa za urembo.

Rais Ruto alisema mswada huo ni muhimu kuongeza mapato ili kufadhili bajeti ya kwanza ya utawala wake ya shilingi trilioni 3.59.

Kamati inayoongozwa na Mbunge wa Molo Kimani Kuria iliazimia ushuru wa 16% VAT kwa bidhaa za petroli, ambayo italeta ushuru wa petroli kwa kiwango sawa na mafuta taa na dizeli.

Kodi iliyopendekezwa ya Ongezeko la thamani (VAT) ilikuwa asilimia 16 na haijarekebishwa hadi kiwango cha chini.

Pia, asilimia tatu ya tozo ya nyumba inayopendekezwa imepunguzwa hadi asilimia 1.5 katika marekebisho mapya.