Babu Owino ajiandaa kumrithi Odinga kisiasa, "Baba amenionyesha njia, sitomuachia yeyote!"

“Viatu vyake ni vikubwa, lakini nitaweka magazeti ndani ndani vinitoshee,” Owino aliongeza akimjibu mmoja aliyemuambia kwamba atatoshea katika viatu vya Odinga.

Muhtasari

• Siasa za mrithi wa Odinga zimeonekana kujipenyeza ndani ya chama cha ODM baada ya kinara wake kutangaza wazi kwamba amejitosa katika mbio za kuwania wadhifa wa Umoja wa Afrika, AU-C.

BABU OWINO na RAILA ODINGA
BABU OWINO na RAILA ODINGA
Image: FACEBOOK

Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino amedokeza kwamba tayari kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ameshampa ishara zote za kuendelea kuongoza chama baada yake.

Kupitia ukurasa wa Facebook, Babu Owino alichapisha picha wakiwa juu ya gari na kiongozi huyo wa chama chake Odinga akiwa ananyoohsea mkono Owino.

Owino alisema kwamba Odinga tayari ameshamuonyesha njia na kumkabidhi kijiti, nafasi ambayo ameapa kutomuachia yeyote kwa gharama yoyote ile.

“Baba amenionyesha njia, siko tayari kuacha hii fursa kwa yeyote,” Owino alinukuu picha hiyo.

Mwanachama huyo wa kudumu wa ODM alisema kwamba japo viatu vya Odinga ni vikubwa katika suala zima la kisiasa, yuko tayari kuvirithi, hata ikimaanisha ni kutanguliza magazeti ndani ili vimtoshee.

“Viatu vyake ni vikubwa, lakini nitaweka magazeti ndani ndani vinitoshee,” Owino aliongeza akimjibu mmoja aliyemuambia kwamba atatoshea katika viatu vya Odinga.

Siasa za mrithi wa Odinga zimeonekana kujipenyeza ndani ya chama cha ODM baada ya kinara wake kutangaza wazi kwamba amejitosa katika mbio za kuwania wadhifa wa Umoja wa Afrika, AU-C.

Odinga ambaye anaonekana kuwa katika nafasi nzuri ya kuteuliwa kama kamishna mwenyekiti mpya wa AU mapema mwaka ujao, anatarajiwa kuondokea siasa za humu nchini, na hivyo kuondoka kama kiongozi wa ODM.

Owino na wenzake wamekuwa wakionyesha nia na dalili za kurithi nafasi hiyo, japo Odinga mwenyewe amewahakikishia mara si moja kwamba bado yuko kwenye usukani na udhibiti wa chama wala hatowaacha pasi na kuwapa mrithi sahihi wa kusongeza mbele maslahi ya chama.