Wanafamilia wa Kiislamu wakamatwa kwa kumchapa mtoto wao kwa kuhudhuria ibada kanisani

Msichana huyo, inadaiwa alichapwa viboko 100 na mjombake huku wanafamilia wengine zaidi ya 6 wakimshikilia kwa nguvu miguu na mikono.

Muhtasari

• Kulingana na sheria za Uganda, katika umri wa miaka 18, mtu huchukuliwa kuwa mtu mzima mwenye haki ya kujumuika ambayo inajumuisha uhuru wa kuabudu.

• Kwa kumpiga Naula, walezi hao walikuwa wakimlazimisha dini yao kinyume na Katiba ya nchi hiyo.

Mwanaume aliyekamatwa
Mwanaume aliyekamatwa
Image: Sagwe

Siku chache baada ya video ya kusumbua akili na macho kwenye jukwaa la X ikionyesha wanafamilia wakimshambulia mtoto kwa viboko kisa kuenda kinyume na dini yao, wanafamilia hao hatmaye wametiwa mbaroni.

Katika video hiyo, familia hiyo inayokisiwa kuwa ya Kiislamu ilirekodiwa ikimpiga viboko mwanao kwa madai ya kuhudhuria ibada kanisani.

Inaarifiwa kwamba tukio hilo lilifanyika katika wilaya ya Kibuku nchini Uganda.

Polisi nchini humo walithibitisha kutiwa mabroni kwa wanafamilia hao Zaidi ya 6 ambapo wanatuhumiwa kwa kumchapa kijana huyo wa kike wa miaka 18 viboko kwa njia ya kikatili.

Msichana huyo ambaye amefahamika kwa jina la Shakira Naula, inadaiwa alichapwa viboko 100 na mjombake huku wengine wakimshikilia kwa nguvu miguu na mikono.

Tabia hiyo imezua hasira kubwa kote nchini humo baada ya video hiyo, iliyorekodiwa na kamera ya simu mahiri, kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii ambapo tangu wakati huo imekuwa ikisambazwa sana.

Naula alidaiwa kutendewa adhabu hiyo isiyo ya kibinadamu kwa kuhudhuria ibada ya kanisa katika Kanisa la Kibuku Prayer Convention Church la Mchungaji Nicholas Kitibwa.

Nile Post wanaripoti kwamba Kikosi cha ulinzi cha Kibuku kilimkamata Bw Higenyi na wajomba wengine watano wa uzazi; Yusufu Nantege, 28, Muhammad Wapesa, 24, Jaberi Lumans, 25, Uthuman Koosu, 25, na Issa Wasereye, 24.

Walezi hao sita waliunganishwa katika mkono wa sheria na Bi Ziyadi Musenero, 29, ambaye msichana huyo aliachwa na mamake anayefahamika kufanya kazi Saudi Arabia.

Bi Musenero ni shangazi wa Naula.

Kulingana na sheria za Uganda, katika umri wa miaka 18, mtu huchukuliwa kuwa mtu mzima mwenye haki ya kujumuika ambayo inajumuisha uhuru wa kuabudu.

Kwa kumpiga Naula, walezi hao walikuwa wakimlazimisha dini yao kinyume na Katiba ya nchi hiyo.